Habari Mseto

Marufuku ya mifuko ya plastiki yaimarisha usafi wa fuo za Lamu

January 29th, 2019 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

MARUFUKU ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imedumu nchini kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa imetajwa kupelekea kuimarika kwa usafi wa fuo za bahari na miji mikuu Kaunti ya Lamu.

Hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaozuru eneo hilo kila kukicha.

Katika mahojiano na Taifa Leo ofisini mwake Ijumaa, Waziri wa Utalii na Viwanda wa Kaunti ya Lamu, Dismas Mwasambu alisema watalii wengi hasa wale wa kutoka ng’ambo wamekuwa wakizuru eneo hilo kwa wingi hasa baada ya kuvutiwa na mazingira safi.

Anasema kukosekana kwa mifuko ya plastiki kwenye fuo za bahari na miji ya Lamu ni changizo kuu ambayo inavutia watalii hao kuzuru Lamu.

“Kinyume na awali ambapo fuo zetu za bahari na miji vimekuwa vikichafuliwa na mifuko ya plastiki, tunashukuru kwamba mwaka mmoja sasa tangu mifuko ya plastiki ipigwe marufuku tumeshuhudia kuimarika kwa usafi. Watalii wengi wamekuwa wakivutiwa na usafi wetu na wanazidi kutembelea eneo hili kwa wingi,” akasema Bw Mwasambu.

Baadhi ya miji iliyotajwa kuboresha usafi wake tangu marufuku ya mifuko ya plastiki kuamriwa nchini ni kisiwa cha Lamu, Shela, Matondoni, Kipungani, Kiwayu na Mkokoni.

Miji hiyo kwa miaka mingi imekuwa vivutio vikuu vya watalii wanaozuru eneo hilo kila mwaka.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Divisheni ya Amu, Philip Oloo, aliwapongeza wakazi wa Lamu kwa kutii marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

Bw Oloo alisema ofisi yake itaendelea kushirikiana na ile ya mazingira kaunti ya Lamu ili kuhakikisha hakuna mtu anayeendeleza utupaji ovyo wa taka hasa zile za plastiki eneo hilo.

“Ninawashukuru wakazi wa Lamu kwa kutii marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki. Tutaendelea kushirikiana na maafisa wa mazingira eneo hili ili kuona kwamba marufuku ya mifuko ya plastiki haikiukwi,” akasema Bw Oloo.