Habari Mseto

Marufuku ya mifuko yaanza rasmi

April 1st, 2019 1 min read

Na WINNIE ATIENO

KUANZIA Aprili 1, 2019, kubeba mifuko isiyosongwa ni marufuku huku serikali ikianza msako wa waagizaji, watengenezaji na wabebaji wa bidhaa hiyo haramu.

Halmashauri ya mazingira nchini (Nema) imeonya kuwa itaanza kusaka kampuni zinazoendeleza utengenezaji wa mifuko hiyo ambayo ni hatari kwa mazingira.

Kulingana na Nema kuanzia Aprili mosi, kubeba mifuko hiyo ni haramu kufuatia marufuku iliyopigwa hivi majuzi.

Nema iliwalaumu watengenezaji bidhaa hizo, huku mkurugenzi mkuu Profesa Geoffrey Wakhungu akisema serikali ilitoa ilani mwaka jana.

“Mlipuuza ilani sasa muda wa kutekeleza wajibu wetu umewadia. Tunawasihi Wakenya watuunge mkono kama hapo awali tulipopiga marufuku mifuko isiyoweza kutumiwa mara nyingi. Kampuni zilikiuka sheria zilipoanza kuunda mifuko sawia na madhara ya plastiki ambayo ni hatari kwa mazingira yetu, mifuko ilikuwa nyembamba sana hata huwezi kutumia mara mbili kubebea bidhaa,” Prof Wahungu alisisitiza.

Alisema yeyote atakayepatikana na mifuko hiyo atakamatwa na kufikishwa mahakamani na kupewa adhabu kali kama ile ya kubeba mifuko ya plastiki.

Prof Wahungu alisema Nema haitolegeza kamba hadi pale mifuko hiyo itaondolewa nchini.

“Hatutawaambia tutaanza misako Mombasa, Nairobi au Nakuru lakini utajuta utakapopatikana na biashara iliyopigwa marufuku, yeyote ambaye ambaye anadhania ni mzaha ajaribu na atakoma,” alionya.