Habari Mseto

Marufuku ya ukataji miti yaongezwa kwa miezi 6

May 24th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imerefusha marufuku ya ukataji wa miti kwa miezi sita, saa chache kabla ya marufuku iliyotangazwa Februari kukamilika.

Marufuku hiyo ya siku 90 ilifaa kukamilika Alhamisi Mei 24. Katika taarifa, Waziri wa Mazingira Bw Keriako Tobiko alisema marufuku hiyo iliongezwa kwa lengo la kutoa nafasi ya uteuzi wa bodi mpya ya Huduma ya Misitu nchini(KFS).

Pia, hatua hiyo itatoa nafasi ya uteuzi wa kamati ya utekelezaji wa mageuzi, “Ili kuongoza utekelezaji wa operesheni za KFS na usimamizi wa sekta ya misitu.”

Marufuku hiyo ni kwa misitu ya umma nay a kijamii, alisema waziri huyo. Mapendekezo ya jopo la uchunguzi lililoundwa kuchunguza matumizi ya misitu na rasilimali yake yanaendelea kutekelezwa, alisema Bw Tobiko.

Hii ni baada ya jopo hilo kutoa ripoti ya mwisho Aprili 30, 2018, kabla ya kuundwa kwa kundi la wataalam kutoa mwelekeo kuhusiana na jinsi mapendekezo hayo yangetekelezwa.

Marufuku hiyo ilitangazwa Februari 24, 2018, kutoa nafasi ya uchunguzi kuhusu usimamizi wa misitu nchini.

Hii ni baada ya malalamishi mengi kuibuliwa kuhusiana na uharibifu wa misitu nchini.