Kimataifa

Marufuku ya virusi vya corona yaondolewa mkoani Hubei

March 24th, 2020 1 min read

Na AFP

BEIJING, China

CHINA imetangaza Jumanne kuwa itasitisha amri ya watu kutotoka nje katika mkoa wa Hubei ambako mkurupuko wa virusi vya corona ulianzia Desemba 2019.

Haya yanajiri huku zaidi ya watu 1.7 bilioni wakiathirika baada ya serikali za mataifa yao kuamuru wasitoke manyumbani katika juhudi za kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.

Wananchi katika mkoa wa Hubei waliruhusiwa kurejelea shughuli zao za kawaida kuanzia usiku wa kuamkia jana, maafisa wa serikali walisema, baada ya wao kusalia nyumbani kwa miezi miwili.

Hata hivyo, wakazi wa jiji la Wuhan ambalo liliathirika zaidi watasubiri hadi Aprili 8 ambapo wataruhusiwa kurejelea maisha ya kawaida.

Kulegezwa kwa marufuku hayo kunajiri baada ya maafisa wa afya nchini China kuripoti Jumatatu kwamba hakukutokea kisa chochote kipya cha maambukizi dhidi ya raia wa nchini; yaani maambukizi ya nyumbani.

Walisema visa 39 vya maambukizi vilitoka mataifa ya nje.

Serikali ilitangaza kuwa baada ya marufuku hayo kuondolewa jijini Wuhan, wakazi watakaobainika kuwa buheri wa afya wataruhusiwa kuendelea na shughuli zao, mradi wawe na kitambulisho rasmi.