Habari za Kaunti

Marungu ya kanjo wa Lamu yazua gumzo

June 6th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

SI jambo geni kuwaona askari wa serikali za kaunti almaarufu kanjo, iwe ni wa kaunti za Mombasa, Lamu, Nairobi, Nyeri, Embu na kwingineko wakishikilia marungu maalum wanapotekeleza majukumu yao.

Ima utasikia malalamishi kwamba kanjo wanakabana koo na hata kuwajeruhi wachuuzi wakitumia marungu hayo wakati kunaposhuhudiwa maandamano.

Mara nyingine utapata hata waumini wa kanisa fulani jijiji wakikabiliana na askari wa baraza na kuishia kutawanywa kupitia matumizi ya marungu wakati kunapozuka tofauti.

Yaani ni kupitia marungu hayo ambapo askari hawa wa mabaraza ya kaunti mbalimbali huweza kutekeleza kazi au majukumu yao vyema.

Lakini ieleweke kwamba kazi ya kanjo si ya kupiga raia.

Ingawa hivyo, kanjo kufanya kazi muhimu kuhakikisha wanazima utozingatiaji wa sheria na amri za miji.

Katika Kaunti ya Lamu aidha, marungu ambayo askari wa Baraza la Kaunti hiyo wamekuwa wakionekana nayo, iwe ni kwenye doria zao za kawaida kisiwani Lamu au wanaposhiriki gwaride kwenye hafla mbalimbali sasa yamekuwa gumzo kwa baadhi ya wananchi eneo hilo.

Hilo linatokana na kwamba marungu hayo ni makubwa mno kiasi kwamba baadhi ya askari, hasa wale wa miili midogo wamekuwa wakionekana wakichechemea, kuweweseka na kutaabika wanapoyabeba au kuyatumia.

Wananchi, hasa kila kunapoadhimishwa hafla mbalimbali, iwe ni za kaunti au serikali kuu, wamekuwa wakisikika wakikejeli askari hao wa baraza la kaunti ya Lamu kwa kile wanachodai ni kubebeshwa mizigo mizito ya marungu.

Bi Amina Omar anasisitiza haja ya Lamu kuibuka na mfumo ambapo askari wake wa baraza la kaunti watapewa marungu saizi ambayo kila mtu inamfaa.

“Haifurahishi kamwe kumuona askari aking’ang’ana kuliinua rungu. Kwa nini hawa watoto wetu askari wa baraza la kaunti tunaowapenda kuachwa kuhangaika na kuchoshwa namna hiyo kazini kwa kubebeshwa marungu makubwamakubwa na mazito? Waipunguze hiyo saizi,” akasema Bi Omar.

Bw Bakari Salim, mkazi wa kisiwa cha Lamu, anahoji kuwa mwonekano wa kanjo wao wakiwa wamemiliki hayo marungu mazitomazito ni suala linalowatia hofu wananchi na hata kufanya wao kuwaogopa.

Askari wa kaunti ya Lamu wakiwa wameshikilia marungu yao. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Salim alisema ni vyema Baraza la Kaunti ya Lamu kufikiria kuwachongea askari wao marungu ya wastani ili wasiendendelee kuogopwa na wananchi kisiwani.

“Yaani ukiona tu huo ukubwa wa rungu tayari fikra zinazokujia kichwani ni madhila wanayoweza kukufanyia hao kanjo endapo watakupata kona mbaya. Askari wetu wa baraza la kaunti watadumishaje urafiki na wananchi endapo silaha wanayobeba inadhihirisha wazi ukatili wao? Kaunti ibadilishe hayo marungu. Yanaleta picha mbaya,” akasema Bw Salim.

Naye Bi Husna Alwy aliwaonya asari wa baraza la kaunti ya Lamu dhidi ya kuyatumia marungu hayo kukabiliana na wananchi.

Bi Alwy alieleza hofu kwamba endapo askari watatumia fimbo hizo kuwapiga wananchi, hilo litakuwa ni sawa na kutekeleza mauaji peupe.

“Hofu yangu ni kuwa chochote kinaweza kutokea. Kwa mfano, maandamano yanapozuka huwa kila mtu anarukwa na akili. Wasiwasi wetu ni hao kanjo wajihami kwa marungu hayo mazito na kisha wayatumie kikweli kuwakabili waandamanaji. Ni wazi marungu hayo mazito yakimwahi mtu kichwani au mgongoni yanamuua. Yabadilishwe,” akachacha Bi Alwy.

Hassan Aboud naye akawasuta askari wa baraza la kaunti ya Lamu, akisema hata wenyewe binafsi wameonekana wazi wakisumbuka, hasa kunapokuwa na maonyesho mbalimbali yanayojumuisha magwaride majukwaani.

Bw Aboud aliwafokea kwa kile anachosema ni kuendeleza kimya wakati wakiumia.

“Kwa nini hawa askari wetu wa baraza la kaunti wanyamazia hali hiyo ambayo ni wazi inawaumiza. Utapata askari akitaabika kabisa katika kujaribu kutekeleza yanayompasa wakati wakiwa jukwaani kuonyesha mbwembwe zao. Endapo fimbo ni za saizi ya wastani, hilo lingewafanya kuwa hafifu kutekeleza majukumu yote kwa wakati wowote,” akasema Bw Aboud.

Akijibu suala hilo, Meneja wa Baraza la Manispaa ya Lamu, Bw Abdulswamad Abdalla alikubali kwamba saizi ya marungu kwa baadhi ya askari wake kweli ni kubwa na yenye uzito mwingi.

Meneja wa Baraza la Lamu Abdulswamad Abdalla. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Abdalla aidha alisema tayari baraza la kaunti ya Lamu limejihami kwa kila saizi ya marungu au fimbo hizo, zote zikiwa zimehifadhiwa kwenye stoo.

Alisema ni changamoto wakati askari wa baraza la kaunti wanapokabidhiwa marungu hayo wakati yanapohitajika kwani hayajanakiliwa kwamba mtu fulani, wa saizi fulani anapaswa kuchukua aina fulani ya rungu.

“Wajua tuko na marungu saizi tofauti tofauti. Kuna ya saizi kubwa na ndogo, ambapo yote tumeyachanganya kwenye stoo moja. Huhitajika wakati askari wetu wanapotekeleza majukumu maalum, hasa kunapotokea maandamano au kukiwa na hafla fulani,” akasema Bw Abdalla.

Akaongeza, “Uhitaji unapotokea huwa marungu yanagawanywa upesi kwa askari wetu, hivyo kwa wale wasiobahatika basi hujikuta wakiwa wamepokezwa marungu makubwa kupita saizi yao ya mwili. Huwa ni bahati mbaya tu.”

Meneja huyo wa Baraza la Manispaa ya Lamu aidha aliahidi kwamba watazingatia lalama za wakazi kwa kuhakikisha askari wa baraza la kaunti wanapewa fimbo au marungu ya wastani ili kejeli kuwahusu zisiendelee.

“Polisi wa Kenya huwa na bunduki maalum mtu anakabidhiwa na hata kuandikishwa wakati fulani kulingana na hali au uhitaji kwa wakati huo. Ila sisi marungu yetu ni yale ya askari kujiokotea au kukabidhiwa tu kutoka kwa stoo yetu. Itabidi tuwe makini na kuzingatia saizi ya wastani ya rungu analokabidhiwa askari husika kama hilo linazua gumzo kwa wananchi wetu watufuku,” akasema Bw Abdalla.