Habari

Marwa ashtakiwa kwa kumdhalilisha Spika

March 6th, 2018 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

MAHAKAMA ya Rufaa imeagiza Katibu Wizara ya Ugatuzi Nelson Marwa ashtakiwe kutokana na madai ya  kumdhalilisha Spika wa Bunge la Kaunti la Mombasa Harub Ebrahim Kharti.

Bw Kharti alimshtaki Bw Marwa mnamo Januari 2017 kwa kumhusisha na ulanguzi wa dawa za kulevya na kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Kukamatwa kwa Bw Kharti kulizua uhasama baina ya Bw Marwa aliyekuwa Mshirikishi wa Ukanda wa Pwani, na Gavana wa Mombasa Hassan Joho. Gavana Joho alivamia afisi za mkoa wa Pwani na kutaka Bw Kharti aachiliwe huru.

Mnamo Machi 14, mwaka 2017, Jaji wa Mahakama Kuu Njoki Mwangi aliamua kuwa Bw Marwa hakufaa kushtakiwa kwa sababu alitoa matamshi hayo kwa niaba ya serikali kama Mshirikishi wa Ukanda wa Pwani.

Mahakama Kuu ilitoa uamuzi huo baada ya aliyekuwa Mkuu wa Sheria Githu Muigai kusema kuwa Bw Marwa hawezi kushtakiwa yeye binafsi kwa kuwa alitamka maneno hayo kama mwakilishi wa serikali.

Mahakama ya Rufaa Jumanne iliamua kuwa matamshi yaliyotolewa yatathibitishwa kuwa yaliambatana na sera za serikali ikiwa kesi dhidi yake itasikilizwa hadi mwisho.