Michezo

Mary Njoroge kusimamia mechi za AFCON U-17

March 13th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MNYANYUAJI kibendera Mary Wanjiru Njoroge ametiwa katika orodha ya wasimamizi 29 watakaopata fursa ya kipekee kusimamia mechi za wanaume kwenye Kombe la Afrika (AFCON) kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Tanzania mwaka 2019.

Hapajatokea katika historia ya mashindano yoyote ya Afrika refa mwanamke kusimamia mechi ya wanaume.

Uamuzi wa kuanza kutumia marefa wa kike katika mashindano ya wanaume ulifikiwa baada ya Kamati ya Marefa ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuwa na kikao Februari 26, 2019 katika makao yake makuu jijini Cairo nchini Misri na kuhudhuriwa na Rais wa CAF, Ahmad Ahmad.

“Hatua hii ni ushahidi tosha kwamba CAF imejitolea kukuza soka ya wanawake. Vilevile, CAF itawapa wanawake usimamizi wa mechi katika mashindano makubwa ili kukuza talanta zao na pia wapate ujuzi katika viwango vya mashindano hasa kwa sababu kuna mechi chache na mashindano machache ambayo mara nyingi kulemeza shughuli zao za kujiendeleza,” CAF imesema katika mtandao wake wa Twitter mnamo Jumatatu.

“Refa Mtanzania Jonesia Rukyaa Kabakama, na marefa wasaidizi Mary Wanjiru Njoroge (Kenya) na Lidwine Rakotozafinoro (Madagascar) ni baadhi ya wasimamizi 29 wa mechi ambao tumechagua kwanza wapate mafunzo mjini Casablanca nchini Morocco kutoka Machi 31 hadi Aprili 4 kupiga msasa ujuzi wao kabla ya mashindano hayo,” CAF imeongeza.

Marefa 15 na wanyanyuaji vibendera 14 kutoka mataifa 25 wanachama watafanyiwa ukaguzi wa kiafya, mazoezi ya uwanjani na pia kufanya mtihani ili tupate orodha ya mwisho ya maafisa wa kusimamia mechi wakati wa mashindano hayo yatakayofanyika nchini Tanzania kutoka Aprili 14-28 mwaka 2019.

Wenyeji Tanzania watalimana na Nigeria, Angola na majirani Uganda katika Kundi A nao Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal wanaunda Kundi B. Timu zitakazofika nusu-fainali zitafuzu kushiriki Kombe la Dunia baadaye mwaka huu.