Mary Nzula Munyao: Mwigizaji chipukizi anayelenga kumiliki brandi ya filamu miaka 5 ijayo

Mary Nzula Munyao: Mwigizaji chipukizi anayelenga kumiliki brandi ya filamu miaka 5 ijayo

NA JOHN KIMWERE

INGAWA hajapata mashiko kwa viwango anavyotarajia ni mmojawapo wa waigizaji wa kike nchini Kenya wanaopania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

Aidha ni mwanadada anayetegemea uigizaji kukimu mahitaji yake kimaisha. Kando na uigizaji dada huyu mwenye tabasamu ya kuvutia hufanya biashara ya kuuza nguo kupitia mitandao ya kijamii pia anamiliki kampuni ya usafiri iitwayo Lodes Safaris.

Mary Nzula Munyao maarufu Kamene kwa jina la usanii kiasi alipuuzia taaluma ya uana habari na kukumbatia uigizaji. Binti huyu amehitimu kwa shahada ya digrii kwenye Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kama mwana habari wa redio na televisheni.

“Nilivutiwa na masuala ya uigizaji nikisoma katika chuo kikuu ambapo baadaye nilijiunga na kikundi cha Raw Talent mwaka 2015 na kuanza kuigiza,” anasema na kuongeza kuwa mtaka cha mvunguni ni sharti ainame.

Mwigizaji anayekuja kwa kasi, Mary Nzula Munyao maarufu Kamene anayelenga kuibuka mwigizaji wa kupigiwa mfano miaka ijayo. PICHA | JOHN KIMWERE

Akifanya na kikundi hicho alishiriki filamu ya ‘My Ndia Nduku‘ iliyofanikiwa kuteuliwa na kutwaa tuzo ya Best Short Film kwenye hafla ya Machawood mwaka 2015.

”Kusema ukweli licha ya kuhitimu kama mwanahabari uigizaji upo kwenye damu maana huwa ninajituma vilivyo bila kulegeza kamba,” akasema.

Kamene amepata umaarufu kutokana na kipindi cha Classmates ambacho huzalishwa na kampuni ya Assignment Studio na kupeperushwa kupitia runinga ya KBC. Kupitia kampuni hiyo pia ameshiriki filamu ya ‘Nganya’ iliyopata mpenyo kupeperushwa kupitia Maisha Magic.

Kadhalika filamu ya ‘Fatal Crush‘ iliyowafikia wafuasi wa maigizo kupitia runinga ya K24.

”Bila kujigamba nimejaa furaha tele kwa kuzingatia kwamba filamu ya ‘Classmate’ ilinipa nafasi kuteuliwa kwenye tuzo za Kalasha International Awards 2021 kitengo cha Best Performance in TV Comedy,” akasema.

Mwigizaji anayekuja kwa kasi, Mary Nzula Munyao maarufu Kamene anayelenga kuibuka mwigizaji wa kupigiwa mfano miaka ijayo. PICHA | JOHN KIMWERE

Kwa waigizaji wa humu nchini angependa kujikuta jukwaa moja na Sarah Hassan ambaye ameshiriki filamu kama ‘Crime and Justice’ pia ‘Zora‘ ambayo hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Anakariri kuwa anatamani sana kutinga hadhi ya mwigizaji wa kimataifa anayezidi kutamba kwenye filamu za Hollywood, Mkenya aliyezaliwa nchini Mexico, Lupita Nyong’o.

Anadokeza kuwa anapenda sana filamu yake iitwayo ’12 Years a Slave’.

”Ufanisi wake umenitia motisha na kudhihirisha kuwa suala la ngozi sio kizingiti cha kutofanya vizuri katika masuala ya uigizaji kimataifa,” anasema.

Lupita amewatia motisha Wakenya wengi hasa waigizaji wa kike wanaokuja ambao kamwe hawajapiga hatua yoyote katika sekta ya maigizo.

Lupita ameibuka kielelezo kizuri kwa waigizaji wengi tu wanaokuja. Amebahatika kuteuliwa kwenye tuzo kibao tangu atwae tuzo ya Oscar Awards mwaka 2012 kupitia filamu ya ‘12 Years a Slave‘.

Lupita amefanikiwa kuteuliwa kuwania tuzo nyingi tu baadhi zikiwa ni Golden Globe Award for Best Supporting Actress, A BAFTA Award for Nest Actress, Screen Actors Guild Awards.

Kamene anashauri waigizaji wenzake nyakati zote wawe wepesi wa kujituma wanapopata fursa kuonyesha ujuzi wao huku wakijiaminia wanaweza bila kujidharau.

Anataka wenzao waliowatangulia kuwashika mkono na kuwapa mawaidha jinsi ya kufanya kazi hii ili kufanikisha azma yao katika tasnia ya uigizaji.

 

  • Tags

You can share this post!

HOKI: Lakers yaendelea kujiimarisha iwe tishio kwa...

Aliyekuwa Rais wa Botswana ajiondoa ghafla kama mwenyekiti...

T L