Mary Wambui Mungai kujua hatma yake Januari 10, 2023

Mary Wambui Mungai kujua hatma yake Januari 10, 2023

NA RICHARD MUNGUTI

HATMA ya Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) Mary Wambui Mungai anayekabiliwa na shtaka la kukwepa kulipa ushuru wa Sh2.2 bilioni itajulikana Januari 10, 2023.

Hii ni kufuatia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji apewe siku 30 kutathmini ushahidi wote katika kesi hiyo ambapo Bi Wambui alishtakiwa na bintiye.

Kupitia kwa wakili Judy Thongori, DPP alimweza hakimu mkuu Mahakama ya Kuamua Kesi za Ufisadi kwamba hajakamilisha kutathmini ushahidi katika kesi hiyo ili afikie uamuzi.

“DPP hajakamilisha kukagua na kutathmini ushahidi wote katika kesi hii ya ukwepaji kulipa ushuru wa Sh2.2 bilioni. Ameomba muda wa siku 30,” Bi Thongori alimweleza Bw Kombo.

Hakimu alielezwa DPP alipokea barua kutoka kwa KRA mnamo Novemba 23, 2022 ikiomba isuluhishe kesi hiyo nje ya mahakama.

“Licha ya kupokea barua kutoka kwa KRA kesi hiyo isuluhishwe nje ya mahakama, bado hatujawasiliana na DPP Noordin Haji kupata maagizo zaidi. Naomba muda wa siku 30 kukamilisha mazugumzo kuhusu kesi hii,” Bi Thongori alimsihi Bw Kombo.

Bi Wambui ameshtakiwa pamoja na bintiye Purity Njoki pamoja na kampuni yao – Purma Holding Limited – kwa kukwepa kulipa ushuru.

Wambui, Njoki na Purma wanakabiliwa na shtaka la kukwepa kulipa ushuru kati ya 2014-2016.

Bw Kombo alikubali ombi la DPP na kuamuru kesi ya Bi Wambui itajwe tena Januari 10, 2023.

Japo mawakili wa Wambui na bintiye ambao ni Nelson Havi na Adrian Kamotho, hawakupinga ombi hilo ila walielezea mshtuko wao kwamba DPP angali anawaza na kuwazua kuhusu suala hilo la kusuluhisha kesi hiyo nje ya mahakama.

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Croatia kwenye mizani ya wauaji...

Raila atofautiana na wanaoepuka siasa kupata ‘maendeleo’

T L