MARY WANGARI: Kenya yahitaji mbinu za kisasa kuboresha miundomsingi

MARY WANGARI: Kenya yahitaji mbinu za kisasa kuboresha miundomsingi

Na MARY WANGARI

MNAMO Alhamisi maelfu ya abiria na waendeshaji magari kwenye Mombasa Road walilazimika kukesha barabarani kutokana na msongamano mbaya wa trafiki.

Hii ni baada ya wanakandarasi husika kufunga kijisehemu cha barabara hiyo inayojengwa ya Nairobi Expressway kwenye eneo la Mlolongo, huku wakiwaacha maelfu ya abiria na waendeshaji magari kung’ang’ania mkondo mmoja.

Hatua hiyo ni kinaya kikuu wakati huu ambapo Kenya inajitahidi kuafikia viwango vya kimataifa kuhusu miundomsingi ya kisasa.

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, usafiri katika barabara ya Mombasa Road, umekuwa jinamizi kuu linalowakosesha usingizi wananchi wanaotumia mkondo huo na nyakati nyingine kuwalazimu kukesha barabarani.

Kwa baadhi ya waliopangisha makazi maeneo hayo, suluhisho limekuwa kuhamia sehemu nyinginezo.Hata hivyo, Wakenya wanaoishi kwenye makao ya kudumu waliyojenga wamejipata katika njiapanda huku wakilazimika tu kuvumilia masaibu yao na kutumai kwamba ujenzi wa barabara hiyo utakamilika haraka iwezekanavyo.

Nairobi Expressway yenye urefu wa kilomita 34 kutoka Mlolongo hadi Westlands, inatazamiwa kuboresha pakubwa mtandao wa usafiri nchini Kenya pindi itakapokamilika.

Barabara hiyo ambayo ujenzi wake umekadiriwa kugharimu Sh64b ilioni na inayotazamiwa kukamilika katika muda wa miezi michache ijayo, inasubiriwa kwa hamu ikizingatiwa kuwa itarahisisha mno usafiri.

Kadri ujenzi huo unavyoendelea, inatamausha mno kuona jinsi Wakenya wanavyozidi kuumia huku wakitumia saa nyingi wakisafiri, muda ambao ungetumiwa katika shughuli za kiuchumi.

Uchovu na masaibu yamekuwa kawaida kwa raia hao wanaolazimika kurauka alfajiri kuenda sehemu zao za kazi au kwenye biashara zao mbalimbali jijini ili kutafuta riziki.

Waziri wa Usafiri James Macharia amekuwa akitoa wito kwa Wakenya kuwa na subira huku akiahidi kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilishwa haraka iwezekanavyo.

Masaibu yanayowakumba Wakenya Mombasa Road yangeweza kuepukika endapo wadau husika wangezingatia kanuni za kimataifa kuhusu shughuli ya ujenzi.

Kabla ya kujenga majengo au barabara, ni sharti mamlaka na wanakandarasi husika wahakikishe kwamba maslahi ya wakazi, abiria na waendeshaji magari watakaoathiriwa na shughuli hiyo yanatiliwa maanani.

Ni bayana kuwa serikali na wanakandarasi husika wamewafeli Wakenya kwa kukosa ubunifu kuhusu mikakati ya ujenzi wa Nairobi Expressway.Kama taifa, ni sharti tutumie mbinu za kisasa kuafikia viwango vya kisasa kimiundomsingi.

Mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

CECIL ODONGO: Azma ya Wanjigi ni mbinu ya ODM kupenya Mlima...

Wataka fidia iwepo viumbebahari wakiwajeruhi