MARY WANGARI: NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha huduma

MARY WANGARI: NHIF yahitaji mageuzi ili kuboresha huduma

NA MARY WANGARI

KATIKA miezi michache ya hivi karibuni, serikali imekuwa ikijitahidi kufanyia mageuzi muhimu Bima ya Kitaifa kuhusu Afya Nchini (NHIF), katika juhudi za kuboresha huduma za afya nchini.

Mojawapo wa mikakati hiyo ni kuanzishwa kwa mfumo wa kuwasajili kielektroniki wanachama 8.9 milioni wa NHIF kwa kutumia alama zao za vidole.

Mfumo huo mpya ambao tayari umeanzishwa katika hospitali za Kaunti za Nairobi, Eneo la Kati, Magharibi, Nyanza, Mashariki na Bonde la Ufa, unadhamiriwa kukomesha udanganyifu na kuboresha malipo ya huduma za matibabu.

Aidha, kuna Mswada wa Kufanyia Marekebisho Bima ya Kitaifa kuhusu Huduma za Hospitali unaopendekeza kuifanya kuwa lazima kwa kila mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kujisajili kama mwanachama wa NHIF ni miongoni mwa mageuzi mapya yanayoendelea.

Juhudi hizi zinastahili kupongezwa na zinaashiria siku njema za usoni ikizingatiwa kwamba afya njema ni kiungo muhimu cha ukuaji na ustawi wa uchumi nchini.

Kando na umuhimu wa afya njema katika kufanikisha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ambao ni mojawapo wa Ajenda Kuu za Maendeleo Duniani, uhalisia ni kwamba, ili taifa lolote liweze kuendelea, ni sharti raia wake wawe wazima kiafya.

Serikali hivyo basi, ni sharti ihakikishe utekelezaji kikamilifu wa sera zitakazowezesha kuwepo kwa huduma bora za afya kwa bei nafuu ambayo kila raia anaweza kuimudu.

Njia mojawapo ya kufanikisha haya ni kupitia ushirikiano wa serikali na mashirika ya kibinafsi yanayotoa huduma za bima ya afya ili kuboresha huduma ya afya nchini kupitia miundomsingi thabiti na vifaa vya matibabu.

Kwa muda mrefu, Wakenya wamejipata taabani baada ya kulemewa na mzigo wa kugharamia matibabu huku wengi wao wakiifilisika hata baada ya kujisajilisha na bima za umma kama vile NHIF.

Si ajabu kwamba wengi wanaojiweza kifedha, wamekimbilia mashirika ya kibinafsi yanayotoa bima za afya wakiwa na hakikisho la kupata huduma bora zaidi japo kwa ada ghali.

Hali kwamba NHIF imekuwa ikibadilisha sheria zake mara kwa mara hata bila ya wanachama wake kutarajia inafanya mambo kuwa magumu hata zaidi.

Mfano mzuri ni kuhusu janga la Covid-19 ambapo NHIF iliamua kusimamisha ghafla utowaji wa huduma za matibabu wakati ambapo wananchi walikuwa wakizihitaji zaidi hasa ikizingatiwa kwamba bado wanaendelea kulipa ada zao kila mwezi.

Ripoti mpya iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti Mashirika ya Bima (IRA) iliashiria kwamba ni asilimia 34.4 pekee ya mapato yaliyokusanywa kutokana na malipo kuhusu bima ya afya mwaka uliopita.

Takwimu hizo zinatofautiana pakubwa na hospitali nyingi za kibinafsi zinazotoa huduma bora za afya ikilinganishwa na hospitali za umma, ambapo ziliandikisha asilimia 80 ya mapato kutokana na malipo ya bima ya afya.

Kulingana na takwimu hizo, ni wazi kwamba serikali ni sharti iwe makini inapotekeleza mageuzi kuhusi NHIF ili kuhakikisha kwamba yatamfaidi mwananchi wa kawaida kinyume na kumwongeza mzigo zaidi.

Ili NHIF iwe na manufaa kwa Wakenya, ni sharti serikali ihakikishe kwamba mageuzi yanayoendelea kamwe hayatahujumu hatua zilizopigwa katika kuboresha bima hiyo ya kitaifa kuhusu afya.

Ni kupitia tu kuwepo kwa wananchi walio wazima kiafya ndipo tunaweza kuunda taifa imara katika kila nyanja.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Si wakati mwafaka wa kuadhimisha ya Siku...

Sifa zinazozolea kanga umaarufu