MARY WANGARI: Tujihadhari hili zimwi la matumizi ya pufya lisitumeze

MARY WANGARI: Tujihadhari hili zimwi la matumizi ya pufya lisitumeze

Na MARY WANGARI

KIMEKUWA kipindi kigumu kwa Kenya chenye hisia mseto tangu Michezo ya Olimpiki ilipong’oa nanga jijini Tokyo, Japan, wiki moja iliyopita.

Kenya ikiongozwa na mtimkaji mwenye tajriba Eunice Sum na naibu kinara wa kikosi cha taifa cha raga ya wachezaji saba kila upande Andrew Amonde ilishiriki hafla ya kufana ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yaliyokuwa yameahirishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku kukiwa na matarajio makuu.

Wiki ya kwanza ya mashindano hayo ilikuwa ya kutamausha kwa Wakenya huku wachezaji wote waliochaguliwa kuwakilisha taifa katika michezo ya raga, taekwondo, ndondi, voliboli na mingineyo wakikosa kufua dafu.

Wakenya walijipa moyo wakielekeza macho yao kwa mashindano ya riadha ambayo katika miaka iliyotangulia, yameshindia taifa hili nishani tele.

Furaha yao ilikatizwa ghafla baada ya mwanariadha mchanga Mark Otieno kuzuiwa kushiriki michezo hiyo almaarufu Tokyo 2020 Olympics baada ya kupatikana na chembechembe za dawa za kuongeza misuli nguvu (pufya).

Ingawa hii si mara ya kwanza kwa wanariadha wa Kenya kufeli vipimo vya pufya au muku, uhalisia ni kwamba suala hilo ni aibu mno na linatia doa sifa ya Kenya kama mababe wa riadha barani Afrika na duniani kwa jumla.

Tukio hilo lilivutia kumbukumbu za miaka miwili iliyopita ambapo marufuku ya bingwa wa mbio za marathon katika Olimpiki 2016, Jemimah Sumgong alipokonywa taji lake na marufuku yake kuongezwa maradufu hadi miaka minane kutokana na matumizi ya dawa hizo za kututumua misuli.

Mnamo 2019, Tume Huru ya Nidhamu ya Shirika la Kimataifa la Riadha (IAAF) iliongeza marufuku ya Sumgong, 34, aliyekuwa mwanamke wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki, kwa miaka minne hadi Aprili 3, 2025.

Hayo yalijiri hata kabla ya Kenya kupata afueni kutokana na aibu kuu iliyoigubika baada ya wanariadha wawili kutimuliwa katika kambi za wanariadha wakati wa kivumbi cha Riadha za Dunia mnamo 2015.

Wanariadha hao walifeli vipimo vya matumizi ya dawa haramu na kufurushwa katika mashindano hayo yaliyokuwa yakifanyika jijini Beijing, China.

Huku tukiwa na matumaini makuu kuhusu timu ya wanariadha wetu wanaotuwakilisha kwenye mashindano hayo jijini Tokyo, hatuwezi kupuuza hoja kwamba suala la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwenye misuli miongoni mwa wanariadha ni tishio kuu.

Inasononesha mno kwa wanariadha kutimuliwa na kurejea nyumbani mikono mitupu na kwa aibu tele baada ya serikali kutumia rasilimali nyingi ambazo zingetumika vinginevyo, kuwafadhili kushiriki mashindano hayo ya kimataifa.

Ni sharti wadau husika wawekeze katika mikakati kabambe ya kuhakikisha wanariadha wanaandaliwa vyema na kwamba wanazingatia sheria na kanuni hasa kuhusiana na matumizi ya dawa haramu, la sivyo Kenya itageuka kuwa dhihaka kwenye ulingo wa spoti.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

CECIL ODONGO: ODM isiingie mkataba kipofu kama wa Nasa

Wapwani wakaushwa tena