MARY WANGARI: Utafiti mpya wahimiza manufaa ya kupokea chanjo

MARY WANGARI: Utafiti mpya wahimiza manufaa ya kupokea chanjo

Na MARY WANGARI

WANASAYANSI wamethibitisha kuwa kuchelewesha upokeaji dozi ya pili ya chanjo ya Covid-19 kwa kiasi cha miezi 10 baada ya kupokea dozi ya kwanza kunaimarisha kinga ya mwili.

Kulingana na utafiti mpya uliofanywa na kundi la wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, kuchelewesha upokeaji dozi ya pili ya chanjo aina ya AstraZeneca kwa miezi kadhaa, kunaongeza idadi ya chembechembe za kinga mwilini.

Kundi hilo lililounda chanjo ya AstraZeneca vilevile liliashiria kuwa, kinyume na kuathirika kiafya, kupokea dozi ya tatu ya AstraZeneca kunasababisha chembechembe zinazokinga mwili ‘kuongezeka pakubwa’ dhidi ya virusi hatari vya corona.

Utafiti huo ni habari njema kwa mataifa maskini ambayo yana uhaba wa chanjo na yanahofia kuhusu ucheleweshwaji wa dozi ya pili na ya tatu, kulingana na kiongozi wa utafiti huo, Andrew Pollard.

Haya yamejiri miezi minne tangu Kenya ilipopokea shehena ya kwanza ya dozi zaidi ya milioni moja za chanjo ya AstraZeneca, miongoni mwa dozi 3.56 milioni ilizotengewa.

Katika awamu ya kwanza ya utowaji chanjo, Wizara ya Afya ililenga maafisa wanaotoa huduma muhimu kama vile wahudumu wa afya, walinda usalama, walimu na wengineo.

Baadaye wazee wenye umri kuanzia miaka 58 na watu wanaoishi na matatizo sugu ya kiafya walipatiwa kipau mbele katika utowaji chanjo hiyo kabla ya kutolewa kwa Wakenya wote.

Mwanzoni, chanjo ya AstraZeneca ilipokelewa kwa shaka na wasiwasi kutokana na habari nyingi za kupotosha kuhusu athari zake.

Ripoti za watu kufa ghafla katika hali tatanishi baada ya kupata matatizo ya kiafya yaliyodaiwa kusababishwa na chanjo zilisambazwa mno mitandaoni hali iliyozua hofu miongoni mwa watu nchini na kimataifa huku wengi wakiisusia.

Ukosefu wa uhamasishaji, kushirikisha umma pamoja na ushindani kati ya chanjo za AstraZeneca na Sputnik ulivuruga mambo zaidi huku wengi wakichelea kuendea chanjo hizo zilizokuwa zimesambazwa katika hospitali mbalimbali za umma nchini.

Hatua ya Rais Uhuru Kenyatta pamoja na viongozi wengine mashuhuri kupokea chanjo hiyo hadharani ilisaidia pakubwa kuvutia imani ya wananchi.

Kufikia Mei 10, awamu ya kwanza ya utowaji chanjo ilipokamilika nchini, jumla ya Wakenya 921,546 walikuwa wamepokea AstraZeneca na 527 kupokea Sputnik miongoni mwa chanjo 1,009,000 zilizokuwa zimesambazwa katika vituo mbalimbali vya afya.

Takwimu hizi zinaashiria kuwa mamia ya Wakenya bado hawajapokea dozi ya kwanza ya AstraZeneca.

Lakini Kwa kuzingatia utafiti mpya, ni bayana kuwa Wizara ya Afya inapaswa kuhakikisha kwamba Wakenya wote wamepata dozi ya kwanza ya AstraZeneca badala ya kutilia maanani zaidi usambazaji wa dozi ya pili ili kukabiliana vilivyo na Covid-19.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Matamshi ya Raila kikwazo kwa azma yake kuwa...

Nani safi kati ya Raila na Ruto?