MARY WANGARI: Uwekezaji zaidi kisayansi na kiteknolojia utatufaidi

MARY WANGARI: Uwekezaji zaidi kisayansi na kiteknolojia utatufaidi

NA MARY WANGARI

KATIKA siku za hivi majuzi, hisia kali zimeibuka nchini na barani Afrika kwa jumla kuhusiana na chanjo ya virusi vya corona ambayo inazingirwa na utata kuhusu mikakati ya kiusalama.

Huku jamii ya kimataifa ikijitahidi kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu janga hilo la kiafya ambalo limeyumbisha dunia, ni bayana kuwa umuhimu wa kuwekeza katika tafiti za kisayansi nchini hauwezi ukasisitizwa vya kutosha.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ya dunia yanayosubiri kwa hamu kupokea chanjo dhidi ya gonjwa hilo ambapo wasiwasi kuhusu mikakati ya kiusalama kwa afya ya umma, umekuwa suala tata.

Tangu janga hilo lilipozuka mapema mwaka jana, imekuwa dhahiri kwamba Kenya ina uwezo wa kuvumbua na kubuni suluhisho za kutatua matatizo yake mbalimbali pasipo kutegemea mataifa ya ulaya kila wakati.

Hali kwamba wanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti kuhusu Matibabu Nchini (Kemri) wanashirikiana na wenzao kutoka mashirika ya kimataifa kuwezesha majaribio ya kwanza ya Covid-19, ni ithbati tosha ya nafasi yetu kama taifa katika kuendeleza utafiti wa kisayansi.

Kwa kuzingatia historia ya majanga mengineyo duniani hasa ya kiafya ambapo Bara la Afrika limekuwa mhasiriwa mkuu hasa katika majaribio ya kimatibabu, inaeleweka kabisa ni kwa nini baadhi ya watu wameingiwa na shaka.

Hata hivyo, inatia moyo sana kuwaona wanasayansi wa Kenya wakiwa sehemu ya juhudi za mataifa ya dunia katika kusaka suluhisho dhidi ya janga hilo, kwa kuunda chanjo ambayo ufaafu wake unasemekana kuwa asilimia 90.

Ikizingatiwa kwamba sayansi na teknolojia ndizo msingi wa maendeleo katika taifa lolote lile, serikali na wadau husika hawana budi kutilia maanani nyanja hiyo ili kuboresha maisha ya wananchi kwa jumla.

Tayari serikali imepiga hatua kupitia Sheria 2013 kuhusu Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi iliyowezesha kubuniwa kwa Hazina ya Utafiti Nchini (NRF), ambayo utekelezaji wake ulioanza 2015, umewezesha maendeleo ya kisayansi, teknolojia na uvumbuzi.

Kupitia kubuniwa kwa sera kabambe, Kenya inaweza kunufaika pakubwa kijamii na kiuchumi kupitia kupitia tafiti za kisayansi kutoka kwa mashirika ya utafiti nchini kama vile Kemri, NRF, ILRI, KFRI na mengineyo.

Wakati umewadia kuimarisha nafasi ya utafiti kisayansi kwa kutengea sekta hiyo raslimali za kutosha na utekelezaji wa sera mwafaka kuambatana na Ruwaza 2030.

Uwekezaji katika raslimali na mikakati mwafaka katika nyanja ya sayansi na teknolojia kutafanikisha utajiri, kuboresha maisha ya wananchi na hata mabadiliko kiuchumi kote nchini.

Kenya ina uwezo wa kusuluhisha matatizo anuai kijamii na kiuchumi ikiwemo kuunda chanjo yake binafsi pasipo kulazimika kusubiri Magharibi, endapo tu itajiimarisha zaidi kisayansi na kiteknolojia.

mwnyambura@ke.nationmedia.com

You can share this post!

Kansa ya lango la uzazi bado changamoto mashambani

CECIL ODONGO: Raila asikate tamaa kuuza sera zake Mlima...