Michezo

Masai alilia haki kwa kutolipwa Sh200,000 alizoshinda 2015

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa mbio za Warsaw Marathon, Gilbert Masai bado analilia haki baada ya kutolipwa zaidi ya Sh200,000 alizoahidiwa na waandalizi wa mapambano mbalimbali aliyoyashiriki na kuibuka mshindi humu nchini.

Mtimkaji huyo kutoka eneo la Mt Elgon amesema amekuwa akiishi maisha ya umaskini kutokana na ulaghai wa baadhi ya watu ambao wanazidi kuchuma nafuu kutokana na udhaifu wa mifumo iliyoko kwenye ulingo wa riadha.

Masai aliibuka mshindi wa Great Green Half Marathon mnamo 2015 kabla ya kutawala riadha za Lari Half Marathon mwaka uo huo humu nchini.

Ingawa hivyo, zaidi ya miaka mitano imepita tangu kuandaliwa kwa mbio hizo na Masai bado hajalipwa hata senti moja.

Alitarajiwa kutia mfukoni Sh150,000 kutokana na ushindi wake wa mbio za Great Green na Sh75,000 kutokana na mbio za Lari Half Marathon zilizomshuhudia akiambulia nafasi ya pili.

“Iwapo ningelipwa fedha hizo, ningekuwa mtu tofauti kabisa hii leo. Iwapo ningewekeza fedha hizi katika mradi mzuri yapata miaka mitano iliyopita, ningekuwa nikiishi maisha ya tija kiasi. Lakini kwa sasa nateseka kwa sababu ya udhaifu wa mfumo uliopo katika uendeshaji wa riadha za humu nchini.

Masai aliyeshiriki mbio za Xiamen Marathon mnamo Januari 2020. alitarajiwa kutetea ubingwa wake wa mbio za Warsaw Marathon mnamo Machi 2020 ila kivumbi hicho kikaahirishwa kutokana na janga la corona.

“Nimejaribu kuwafuatilia waandalizi wa mbio za Lari na Green bila mafanikio. Kufikia sasa, nimewasilisha malalamishi yangu rasmi kwa Kituo cha Polisi cha Kiambu na Chama cha Wanariadha Nchini (AK).