Michezo

MASAIBU: Staa mashakani kwa kukejeli kocha

March 20th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

MCHEZAJI nyota, Cristiano Ronaldo wa Juventus ameshtakiwa na UEFA kwa kushangilia visivyo ushindi wa klabu yake dhidi ya Atletico Madrid majuzi katika pambano la Klabu Bingwa barani Ulaya.

Mshambuliaji huyo alionekana akikejeli kocha wa Atletico, Diego Simeone, huku akiwageukia mashabiki wa klabu hiyo na kujishika sehemu zake za siri.

Staa huyo alifanya kitendo hicho baada ya kufunga mabao yote matatu katika ushindi wao wa 3-0, na sasa UEFA imepanga kutoa uamuzi wa kesi hiyo hapo Machi 21 kabla Juventus kukutana na Ajax Amsterdam katika robo-fainali.

Alipokuwa na Real Madrid na kupiga hat trick, aliiwezesha klabu hiyo kuingiza jumla ya Sh81 bilioni.

Katika mechi ya majuzi dhidi ya Ateltico, Mreno huyo alifunga hat-trick kusaidia klabu yake kupindua matokeo ya awali ya kichapo cha 2-0 kutoka kwa Atletico katika mkondo wa kwanza.

Fowadi Cristiano Ronaldo wa Juventus asherekekea baada ya kufunga mabao yote matatu kwenye kabiliano kali la Juve dhidi ya Atletico Madrid ambapo wenyeji walishinda 3-0 Machi 12, 2019, mjini Turin. Picha/ AFP

Kila timu inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inapata pesa, lakini zinazidi kupata pesa nyingi zinapoendelea kupiga hatua.

Timu za Uhispania zilishapata asilimia kubwa ya mgao wa pesa kulingana na orodha iliyotolewa mwaka 2018.

Kwa sababu Atletico walimaliza juu ya Real Madrid, pasi mgao wao utakuwa mkubwa kuliko Madrid maarufu kama Los Blancos ambao walibanduliwa mapema.

Lakini hata baada ya kutolewa na Ajax Amsterdam, Madrid bado inaendelea kupata mkwanja wake.

Hii ni kutokana na sababu kwamba msimu uliopita ligini, Ronaldo alikuwa kwenye kikosi cha timu hiyo ya Uhispania.

Messi ammiminia sifa

Mpinzani wake mkuu, Lionel Messi ni miongoni mwa wanaoendelea kumsifu staa huyo kwa kuibeba Juventus hadi hatua ya robo-fainali.

“Kutokana na matokeo pamoja na mchango wake binafsi, kamwe mashabiki wa Juventus na dunia nzima itamkumbuka milele. Nadhani kile kilichotokea siku hiyo, Ronaldo amethibitisha yeye ni matata kwelikweli,” alisema nyota huyo wa FC Barcelona ambao wamepangiwa kucheza na Manchester United.

“Watu wengi, nikiwemo walidhania Atletico wangekuwa wagumu kumbana, lakini alikuwa na usiku bora kabisa kuliko wenzake na akafunga mabao matatu ya kuokoa timu yake,” aliongeza Messi.

Ronaldo alikuwa katika ubora wake katika mechi hiyo ambayo imemweka pazuri kwenye kampeni za kufukuzia taji lake la tano kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

United waliibandua Paris Saint-Germain wakitarajia kupata mteremko, lakini wameshtuka na kilichotokea kwenye droo ya upangaji wa mechi za robo-fainali.

United wamepangiwa kukutana na Barcelona, na sasa tatizo lao kuu ni jinsi ya kumzuia Messi ambaye walinzi wengi wanamwogopa.

Timu hizo zimekutana mara 11, ambapo United wameshinda mara tatu, sare nne na kupigwa mara nne ikiwemo fainali mbili, mnamo 2009 na 2011.

Kwenye mechi hizo, mabao 35 yamefungwa, Barcelona walifanikiwa kufunga mabao 20 na United 15.