Dondoo

Masaibu tele polo kutorokwa na mke, halafu kimada pia akamtema


NJERIAN, BOMET

JOMBI mmoja wa eneo hili alisadiki maana ya methali maarufu kwamba ukistaajabu ya Musa Utayaona ya Firauni baada mkewe wa ndoa kumtoroka halafu kimada wake wa pembeni naye akamtema.

Inasemekana mkewe jombi aliamua kufungasha virago na kurudi kwa wazazi wake baada ya kugundua kuwa mumewe alikuwa na mpenzi wa pembeni.

Baridi ilipomkabili, jamaa akaamua kuhamia kwa kimada akiamini atapokelewa kwani amekuwa akilipa kodi ya nyumba na kumtimizia mahitaji mengine ya kimsingi.

“Alipofika, mrembo alimtaka acheze mbali akimwelezea wazi wazi kuwa hakuwa tayari kuishi kama mke kabla ya kuvikwa pete,” mdaku akaarifu.

Jamaa hakuwa na budi ila kurudi kwake akijutia tamaa zake.

Jaribio la kumsihi mkewe arudi nyumbani ziligonga mwamba kwa kuwa hii haikuwa mara ya kwanza kuchovya kwenye buyu la asali la wengine.