Makala

Masaibu ya Aisha Jumwa ndani ya ODM

March 5th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Malindi, Aisha Jumwa kwa sasa anatembea kwenye barabara telezi kisiasa baada ya chama chake alichowania nacho kumtimua Ijumaa wiki jana.

Hili lina maana kuwa, ikiwa hatatafuta mbinu ya haraka na ya uhakika ya kujinasua kutoka mtego ambao unamwandama, mtego ambao unaweza ukaishia kuwa kitanzi chake kisiasa, huenda aangamie.

Maji yakizidi unga katika hali hii, huenda Bi Jumwa ajipate akirejea kwa debe tena kutetea wadhifa wake katika uchaguzi mdogo, chama chake cha ODM kikitarajiwa kumnyima tiketi ya uwaniaji.

Haijulikani ni wapi Bi Jumwa alikosana na uongozi wa ODM kwa kuwa alijipa umaarufu wake mkuu kupitia shabaha ya kimaneno akilenga serikali ya Jubilee kuiangamiza, akiwa jenerali sugu wa Bw Raila Odinga na ODM.

Kile kinachojulikana ni kuwa alibadilika ghafla, akaanza kusuta uongozi wa ODM na mikakati yake yote ya kisiasa eneo la Pwani ikageuka kuwa nyimbo za wasifu kwa Naibu Rais, William Ruto.

Amekuwa akikariri kuwa liwe liwalo, amejiunga na merikebu ya Dkt Ruto ya kuwania urais 2022 na hilo halijawapa wakubwa wake ndani ya ODM raha.

Tangu aingie katika siasa akiwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kilifi katika uchaguzi wa 2013, amekuwa mwingi wa hotuba za kukemea serikali ya Jubilee, na kubadilika kwake ghafla ndiko kumewaacha wengi wakiwa hawaelewi.

Shida ni kuwa, ufasaha wake wa lugha na wingi wa mafumbo ya kipwanipwani humpa hata kinga ya kutojibiwa na baadhi ya wanawake wanaoghasika lakini wasiwe na lolote la kufanya.

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ahutubia wakazi wa Mbuzi Wengi, Malindi, Kilifi mnamo Februari 2, 2019. Picha/ Maktaba

Awali akiwa mfuasi sugu wa siasa za Raila, katika uchaguzi wa 2017 aliwashangaza wengi alipoamua kuwania ubunge wa Malindi na akatwaa wadhifa huo kwa urahisi kwa tiketi ya ODM ndani ya Nasa.

Kuhusu kuzaliwa kwake, inaelezwa tu ni miaka ya 70 na ndoa kwake ni habari zake za siri ingawa kuna wale watakuambia moja au mawili kuhusu uhusiabno wake na uchumba.

Cha kueleweka ni kuwa, amekiri hadharani kuwa ni mama ya mtoto mmoja tu wa kiume.

Bi Jumwa amejipata taabani na hali yake ya usemi na ulengaji shabaha kwa maneno mazito na makali.

Mwaka wa 2016, alijipata ndani ya seli katika kituo cha polisi cha Muthaiga baada ya kuhusishwa na matamshi yaliyosawiriwa kuwa ni ya ovyo akilenga utawala wa Jubilee.

Alipoachiliwa, alitangaza kuwa alihangaika kwa siku nne kubakia na nguo zilezile alizokamatwa akiwa amevaa.

“Hebu imagine (tafakari) mwanamke akikaa na chupi moja kwa siku nne!” akagadhabika akijishaua kwa dharau na kejeli kwa maafisa wa usalama na serikali ya Jubilee.

Ingawa alisema kuwa kituo hicho kilikuwa na maji ya mfereji na walikuwa wakikubaliwa kuoga, Jumwa aliteta kuwa simiti ya seli hizo ilikuwa baridi ajabu na mara kwa mara alikuwa akitembelewa na ndoto mbovu.

“Na ndio nimeahidi kuwa hivi karibuni nitarejea katika kituo hicho na nigharamie ukarabati wa seli hizo ili ziwe za kukubalika kwa maisha ya binadamu akiwa anazuiliwa hapo. Hizo seli hata hazifai kutumika na jambazi,” akasema.

Hata hivyo, hadi leo hii, Bi Jumwa hajatimiza ahadi yake ya kurejea kukarabati seli za kituo hicho.

Kuzaliwa

Jumwa ametajwa kuwa ni mzawa wa eneo la Takaungu, Kaskazini mwa Kilifi lakini alihamia eneo la Kakuyuni, Malindi ambapo alijinunulia shamba na akajijengea nyumba.

Hakuna thibitisho kuwa aliolewa na mvuvi katika maisha yake lakini wakatengana alipofanikiwa kutwaa wadhifa wa ubunge.

Jumwa ameorodheshwa katika habari za bunge kuwa alisomea shule ya msingi ya Takanga na baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta University of Agriculture & Technology (JKUAT.)

Kasomea taaluma gani, haisemwi; akamaliza mwaka gani haisemwi pia.

Sio mgeni na patashika mitaani kwa kuwa amekuwa katika maandamano mengi ya mrengo wa Nasa na amekuwa mteja wa mikebe ya vitoa machozi na kutoroka virungu vya maafisa wa polisi.

Kukikaribia uchaguzi mkuu wa 2017 Jumwa alijipata ameitwa na maafisa wa uchunguzi wa Jinai akahojiwe kuhusu madai ya kutisha kumuua mwandani wake wa kisiasa, Ezra Biddi.

Ni madai aliyokanusha na akasema Biddi alikuwa akilenga kumtapeli fedha za kampeni huku akiwa tayari amehamishia uungaji mkono wake kwa mpinzani wa kisiasa eneo hilo.

Hadi siku yake ya kutemwa nje, alikuwa amepewa nafasi tele za kujitetea lakini katika hotuba zake za hadhara, akawa hana haja na maridhiano, akimlenga Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho kama aliyekuwa akichochea masaibu yake.

Awali alikuwa anapendwa sana na Raila kwa kuwa hakuwa akichelea kujumuika miongoni mwa walio waaminifu zaidi na walio na ujasiri wa kumenyana na mawimbi ya Jubilee bila kushurutishwa.