Makala

Masaibu ya chokoraa wakati wa kafyu

June 4th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Kwa zaidi ya miezi miwili iliyopita, Kenya imekuwa ikitekeleza kafyu ya usiku, inayoanza saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi.

Amri hiyo iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta, ilianza kutekelezwa Machi 27, 2020, ili kuzuia msambao wa Covid – 19 baada ya Kenya kutangazwa kuwa mwenyeji wa ugonjwa huu, visa vya maambukizi vikiendelea kuongezeka kila uchao.

Mikakati mingine iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia ueneaji wa virusi hatari vya corona ni pamoja na amri ya uvaliaji maski mtu akiwa katika maeneo ya umma, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake na kunawa mikono kwa sabuni au vitakasa mikono kila wakati ili kuua virusi hivyo.

Mtaa wa Githurai ulioko kiungani mwa jiji la Nairobi, ni wenye shughuli chungu nzima za biashara na uchukuzi kila siku. Sawa na mitaa mingine, mtaa huo pia una jamii ya familia ya watoto wa mitaani ambao kwa sababu zisizoweza kuepukika na wengine kutoroka makwao, kwa ajili ya unyanyapaa walijipata humo.

Hata ingawa kuna kadhaa wakaidi na watundu waliotoroka kwao licha ya kuwa na wazazi, kuna wengine mayatima.

Kati ya saa kumi na mbili hadi saa moja kasorobo, jioni, watu huwa katika pilkapilka za kurejea nyumbani ili kuwahi saa za kafyu ya kitaifa.

Ni kafyu ambayo licha ya kupigiwa upatu kusaidia kudhibiti usambaaji wa Covid – 19, imejiri na lawama chungu nzima maafisa wa polisi wakinyooshewa kidole kwa kutumia nguvu kupita kiasi wanapoitekeleza, kusababisha maafa na hata majeraha kwa wanaoikiuka.

Ni malalamishi ambayo ni kilio cha jamii ya watoto wa mitaa Githurai, na pia mitaa mingine Nairobi.

Katika mtaa huo, jua linapotua na kafyu kubisha hodi, vikosi vya pamoja vya usalama, vinavyojumuisha wale wa kukabiliana na ghasia ndio GSU, hukita kambi. Kwa wanaochelewa kuwa kwenye nyumba kabla ya saa moja, jawabu huwa “mguu niponye”.

Tangu kafyu hii ianze kutekelezwa miezi miwili iliyopita, imekuwa mahangaiko kwa watoto hao wa mitaani, maarufu kama chokoraa. Mchana huwa raha kwao, sawa na mfungwa anapomaliza kuhudumu kifungo cha jela, usiku unageuka kuwa majonzi.

“Kafyu ilipong’oa nanga, wengi wetu tulipitia unyama chini ya maafisa wa polisi. Jioni, ikizingatiwa kuwa hatuna mahali maalum kuita kwetu kulala tulitendewa unyama kwa kupigwa kikatili,” anaeleza mtoto mmoja wa mtaa huo anayejitambua kama Njuguna.

Kulingana na Njuguna, licha ya visa vya polisi kuhangaisha raia wakati wakitekeleza kafyu kuangaziwa na vyombo vya habari na wadau husika kama vile mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, bado jamii ya watoto wa mitaa ingali inapitia dhuluma chini ya maafisa wanaoshika doria. “Tunashangaa ni corona wanasaidia kuzuia kusambaa au ni kuonyesha umahiri wao katika vita kwa kupiga raia?” kijana Njuguna, 14, anahoji.

Mapema wiki, wakazi wa eneo la Bondeni, mtaa wa Mathare, waliandamana kulalamikia unyama wa maafisa wa polisi, baada ya kuua mtoto mmoja wa mtaa aliyetambulika kama Vaite. Inasemekana alipigwa risasi na maafisa waliokuwa wakishika doria wakati wa kafyu.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi punde ya Mamlaka Huru kutathmini Utendakazi wa Polisi, IPOA, taangu kafyu ianze kutekelezwa nchini maafisa wa polisi wameua watu wapatao 15.

Awali, kabla ya janga la Covid – 19 kutua nchini, chini ya mzunguko wa barabara ya Thika Super Highway ulioko mtaa wa Githurai, usiku ulikuwa makao ya watoto wa mitaa mtaa huo kulala. Ila sasa eneo hilo usiku ni mahame, ni marufuku.

Ni hatua ambayo imewaletea mahangaiko chungu nzima. “Mwanzoni, kabla mambo kuharibika tulikuwa tukiungana na kuchangana Sh50 kila mmoja kila siku, tunakodi chumba kulala. Lojing’i zilifungwa, mchana tunashinda vyema, usiku ni kwa neema ya Mungu,” anaelezea kijana Jose, mmoja wa watoto wa mitaa mtaani Githurai.

Janga la Covid – 19 limeathiri uchumi na sekta mbalimbali kwa kiasi kikuu, na kulingana na Jose wanahisi makali ya athari. “Tulitegemea mapato ya kuzolea wafanyabiashara wa vibanda taka na pia pesa tunazopewa na wasamaria wema, ila sasa kuyapata ni vigumu,” anasema.

Kulingana na watoto tuliozungumza nao, wengi wao wamegeuza vibanda vya wafanyabiashara wa masoko ya Githurai kuwa makao ya muda usiku, kulala na kuvumilia kijibaridi kikali. “Muda wa kafyu unapotimu, tunatandaza magodoro au makatoni angalau tupate lepe la usingizi,” wakadokeza.

Vibanda visivyofunguliwa mchana, pia hulala kuondoa maruerue ya kutopata usingizi usiku kucha, (kwa mujibu wa picha kadhaa tulizonasa na kuchapisha na makala haya). “Si wengi wanakubali tushinde katika vibanda vyao mchana kutwa,” akasema mtoto mwingine wa mitaa eneo hilo.

Mbali na vibanda vya masoko, mahandaki yaliyo katika barabara kuu ya Thika Super Highway, pia wameigeuza kuwa makao ya muda usiku. Kulingana na Antony Kabue, mkazi na mfanyabiashara Githurai ambaye mara kwa mara hujitolea kuwasaidia kwa mahitaji ya kimsingi, kama vile chakula, ni katika mahandaki yayo hayo watoto wa mitaa wa jinsia ya kike hujifungulia na kulea watoto.

“Si kisa kimoja au viwili nimeshuhudia kadhaa kujaaliwa watoto. Wanawalelea katika mahandaki hayo. Wanapitia masaibu chungu nzima, serikali ibuni mikakati kusaidia watoto wa mitaa si tu hapa mtaani Githurai ila katika mitaa mingine nchini. Wengi wao ni wachanga, wanahitaji kupata masomo wajiimarishe kimaisha na kimaendeleo,” Kabue akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano ya kipekee.

Licha ya changamoto zinazozingira watoto hao wa mitaa, wanaulimiwa kuchafua mazingira haswa kwa kuenda haja katika vibanda vya wafanyabiashara na pia katika eneo la mapumziko la mzunguko Thika Road, Githurai.

Isitoshe, kadhaa wamehusishwa na visa vya uhalifu, hususan kupora wapitanjia simu na hata pesa.

Tetesi zimeibuka kuwa baadhi yao wamepelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia, ndivyo ‘Rehab’, ila wanatoroka.

Huku Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa wiki hii akitarajiwa kutoa hatma ya baadhi ya masharti kudhibiti msambao wa Covid – 19, ombi la watoto hao ni kafyu iondolewe angalau wapate afueni dhidi ya dhuluma za polisi wanapoitekeleza.