Habari Mseto

Masaibu ya Mwangaza: Maafisa wa DCI wavamia maboma yake

January 7th, 2024 2 min read

NA GITONGA MARETE

MAAFISA kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumamosi, Januari 6, 2024 walivamia makazi rasmi ya Gavana wa Meru Kawira Mwangaza ili kukusanya ushahidi kuhusu mauaji ya mwanablogu Daniel Muthiani, almaarufu Sniper.

Wakiongozwa na mkuu wa kitengo cha mauaji katika makao makuu ya DCI Martini Nyuguto, maafisa hao walishinda katika makazi hayo yaliyoko mtaa wa Milimani mjini Meru ambapo hamna aliyeruhusiwa kuingia wala kuondoka.

Wapelelezi hao walionekana wakiingia na kuondoka katika makazi hayo na Gavana Mwangaza lakini DCI haikufichua aina ya ushahidi ambao walitaka.

Hata hivyo, mshrikishi wa DCI eneo la Mashariki, Bw Lenny Kisaka alisema maafisa hao walikuwa wakikusanya ushahidi wa kusaidia katika uchunguzi wa mauaji hayo.

Aliongeza kuwa maafisa hao watatembelea sehemu nyingine kadhaa kusaka ushahidi.

“Tunaendesha uchunguzi kuhusiana na mauaji ya mtu maarufu anayejulikana kama Sniper na tumezuru sehemu kadhaa. Tumeleta kundi la wachunguzi wataalamu wa aina mbalimbali za uhalifu,” Bw Kisaka akaambia wanahabari nje ya makazi ya Gavana Mwangaza.

“Hii ni sehemu ya mchakato unaoendelea kukusanya maelezo yoyote kuhusiana na mauaji tunayochunguza,” Bw Kisaka akaongeza.

Katibu katika serikali ya Kaunti ya Meru, Dkt Kiambi Athiru alikuwa pamoja na Bw Kisaka akieleza kuwa aliitwa “kuwasaidia maafisa wa upelelezi kufikia sehemu mbalimbali wakati wa uchunguzi wao.”

Maafisa wa DCI walivamia nyumbani kwa Gavana Mwangaza siku mbili baada ya kaka yake Bi Mwangaza, Murangiri Kenneth Guantai kukamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya Muthiani ambaye pia alikuwa mwanaharakati wa kisiasa Meru.

DCI imeomba kumzuilia, pamoja na washukiwa wengine watano, kwa siku 21 ili kutoa nafasi kwa uchunguzi zaidi.

Katika ombi lililowasilishwa katika Mahakama ya Kiambu mnamo Ijumaa (Januari 5, 2024), DCI pia inataka kuwazuilia wafuatao; Kenneth Mutua Matiri, Fredrick Muriuki Kiugu, Frankline Kimathi, na Timothy Kinoti.

Guantai pia anahudumu katika kikosi cha walinzi wa Gavana Mwangaza, huku Mutiri akihudumu kama afisa wa itifaki katika afisi ya mkuu huyo wa Kaunti ya Meru.

Mshukiwa mwingine ni Vincent Murithi Kirimi ambaye inadaiwa alimpigia simu Muthiani kabla ya kutoweka kwake.

Mwanablogu huyo alitoweka Desembe 2, 2023 na mwili wake ukapatikana msituni kando ya Mto Mutonga, Tharaka Nithi mnamo Desemba 16, 2023.

Gavana Mwangaza ameponea pembamba mara mbili kutimuliwa uongozini.