Kimataifa

Masaibu ya wanahabari UG uchaguzi ukijongea

December 13th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KAMPALA, Uganda

WANAHABARI nchini Uganda wamelalamikia amri ya Baraza la Vyombo vya Habari la Uganda kuwataka wanahabari wote wajisajilisha upya na baraza hilo.

Wanahabari hao wamesema kwamba hatua hiyo imejiri wakati usiofaa pasipo kuwapa muda wa kutosha kujiandaa.

Kulingana na Shirika la Wahariri, muungano unaowaleta pamoja wahariri, matakwa ya kuwasajili wanahabari yametolewa katikati mwa kampeni za uchaguzi, wakati wanahabari wengi tayari wako mashinani kufuatilia kura hiyo.

Uchaguzi wa urais utafanyika Januari 14, 2021, huku Rais Yoweri Museveni akiwania kwa awamu ya sita baada ya kuwa mamlakani kwa miaka 34. Mpinzani wake mkuu ni msanii na mwanasiasa Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine.

Kwa mujibu wa masharti yaliyotolewa na Baraza hilo mnamo Alhamisi, wanahabari wote wanaofuatilia shughuli za uchaguzi wanapaswa kuonyesha vitambulisho vya uanahabari kutoka kwa Baraza, la sivyo hawataripoti kuhusu uchaguzi au shughuli nyinginezo.

Shughuli hiyo inayoanza wiki ijayo, itaendelea hadi Disemba 21.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyombo vya Habari Uganda, Paulo Ekochu, alisema kupitia taarifa kwamba hatua hiyo inadhamiriwa kuhakikisha sekta hiyo imedhibitiwa vyema bila kuwepo kwa wanahabari ghushi.

Hata hivyo, Kituo cha Afrika kuhusu Ubora wa Vyombo vya Habari (ACME), kinasema masharti hayo mapya si ya kutiliwa shaka tu bali pia yanazua maswali.

“Tunahofia hatua hiyo, wakati huu ambapo wananchi wanahitaji kupata habari za kuaminika ili kufanya maamuzi thabiti. Kazi ya Baraza ni kuwasajili wanahabari halali katika “sajili ya wanahabari Uganda” ambapo wale wamelipa ada inayohitajika wanapewa leseni ya kufanya kazi,” ilisema taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa ACME, Peter Mwesige.

Shirika la Wahariri limehimiza Baraza hilo kufanya majadiliano zaidi na wadau ili kuhakikisha haki ya kikatiba ya raia kupokea habari haiathiriwi.

Haya yamejiri wiki chache tu baada ya serikali ya Uganda kufurusha wanahabari watatu wa Canada.

Akifafanua hatua hiyo, Msemaji wa Serikali Ofwono Opondo alisema wanahabari hao wa kituo cha umma nchini Canada: Margaret Evans, produsa Lily Martin na mwanahabari wa video JeanFrancois Bisson, walitimuliwa kwa kukiuka kanuni za hati za usafiri.

“Walijisajili kwa cheti cha watalii kwenda kuzuru Mbuga ya Bwindi wilayani Kanungu, kisha wakapatikana katika hoteli ya Sheraton mjini Kampala wakifanya makala kuhusu siasa na Covid-19. Ili kufanya hivyo, ni sharti ujitangaze kama mwanahabari,” akaeleza Bw Opondo.