Makala

Masaibu ya wanamuziki na maprodusa kipindi hiki cha corona

September 25th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MAINA Mwangi amekuwa katika ulingo wa sanaa kwa muda wa miaka kadhaa, kazi ambayo amekuwa akiitegemea kukidhi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Ni produsa na pia mwanamuFziki, muimbaji wa nyimbo za injili. Shughuli ya kupalilia wasanii chipukizi, kupitia studio yake alikuwa akiiendeshea eneo la Zimmerman.

Hata hivyo, Kenya ilipothibitisha visa vya Covid-19, mambo yalichukua mkondo mwingine.

Kanuni na mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia kuenea kwa corona, Mwangi anasema ilichangia biashara yake kuathirika kwa kiasi kikuu.

“Mikusanyiko ya watu ilipopigwa marufuku, nililazimika kufunga studio yangu,” anadokeza produsa huyo.

Wizara ya Afya inaendelea kusisitiza mikusanyiko ya watu ingali marufuku, licha ya baadhi ya viongozi na wanasiasa kuonekana wakiandaa mikutano ya umma, inayohudhuriwa na mamia na maelfu ya watu.

Ni sheria na mikakati ambayo imetatiza biashara nyingi, kuanzia sekta ya hoteli na utalii, uchukuzi, vyombo vya habari, kilimo na elimu…na kuchangia kuyumba kwa uchumi.

Kufanikiwa na kuimarika kwa maprodusa, kunategemea kuwepo kwa wanamuziki. Ikizingatiwa kuwa wasanii wengi hutegemea mialiko ya mikusanyiko ya umma, ikiwemo makanisa na hafla za harusi, kutumbuiza ili kuvuna mapato, marufuku ya makongamano ya watu imefunga mianya ya wasanii kujiendeleza kimaisha.

Wanjiku Gitau, mwimbaji wa nyimbo za injili anasema mara ya mwisho kutumbuiza katika hafla ilikuwa kabla ya Machi 2020, Kenya ilipoandikisha kisa cha kwanza cha Covid-19.

Wanjiku Gitau (kulia) akiwa studioni. Picha/ Sammy Waweru

“Haijakuwa rahisi katika sekta ya usanii, hasa iwapo mwanamuziki hana kazi ya ziada kujiendeleza kimaisha,” Wanjiku ambaye pia ni mfanyabiashara anaelezea.

Ni athari ambazo maprodusa wengi wanazihisi, kiasi cha kushurutika kufunga studio zao. “Imekuwa vigumu kuendelea kulipa kodi ya studio ambayo haiingizi mapato,” produsa Mwangi akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Akiwa mume na baba, alisema amekuwa akitegemea vibarua vya ziada na pesa alizokuwa ameweka kama akiba. “Ala za kazi nilizipeleka ninakoishi na familia yangu. Kualika msanii au wasanii kurekodia nyimbo katika mazingira hayo, si jambo la kuridhisha,” anasema.

Huku Rais Uhuru Kenyatta akisubiriwa kuhutubia taifa mapema juma lijalo, wasanii hao na ambao wanawakilisha sauti za wenzao, wana ombi kwa kiongozi wa nchi: “Tunakusihi utufungulie uchumi, legeza masharti uliyoweka na yanayoathiri wasanii na sekta ya biashara kwa jumla, kati ya sekta nyinginezo.”

Kwa hakika, imekuwa kinaya kuona viongozi na wanasiasa wakihutubia halaiki ya watu katika mikutano ya umma, ilhali viongozi haohao walioko serikalini ndio wamepiga marufuku mikusanyiko.

Katika kipindi cha muda wa wiki kadhaa zilizopita, mfululizo, maambukizi ya Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni janga la kimaitaifa, yameonekana kushuka.

Wakenya wengi wana matumaini hotuba ya Rais Kenyatta italeta afueni, alegeze zaidi kanuni na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Katika ulingo wa sanaa, wasanii tuliozungumza nao wanasubiri kwa hamu kuona iwapo Rais atalegeza kamba masharti ya sekta wanazotegemea, wakisema wako tayari kutii maelekezo yatakayotolewa.