Makala

Masaibu yamsukuma kuishi kwa nyumba ya wazee

August 21st, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

KAWAIDA mtu yeyote anaposikia kuhusu nyumba ya wazee, kitu cha kwanza kitakachomjia akilini ni picha ya watu wakongwe sana, ambao hata wengine hawawezi kutembea bila kusaidiwa.

Mara kwa mara, wazee hawa huwa wametelekezwa na jamaa zao au wamepelekwa katika nyumba hizo kwa kuwa familia zao hazina uwezo wa kuwaangalia vizuri siku zao za uzeeni.

Lakini akiwa na umri wa miaka 41 pekee, Bi Caroline Awuor amelazimika kuishi katika makazi ya wazee ya Alms, ilio katika wadi ya Tudor, Kaunti ya Mombasa.

Makazi hayo ya Alms yalianzishwa mwaka wa 1924 na ni mojawapo ya nyumba zee ya wazee nchini.

Unapomtazama, Bi Awuor bado ana nguvu kama mtu yeyote mwenye umri huo na anatembea wima, kwa kifupi, si mkongwe.

Katika kituo hicho kuna wazee 21 na mkongwe zaidi ana umri wa zaidi ya miaka 100 na ule wa chini miaka 41, ambaye ni Bi Awuor.

Basi, ilikuwaje hadi akaishi katika nyumba hiyo ya wazee? Bi Awuor anasimulia kuwa jamaa zake walimtema kwa kuwa ana maradhi ya kifafa.

Alisema kuwa alilazimika kulala kando ya barabara kwa muda mrefu kabla ya kupelekwa katika makazi hayo na mama mmoja aliyemfahamu.

“Sina mahali pa kuita nyumbani wala wazazi wa kutegemea kwa kuwa mimi ni yatima. Hata hivyo, hali yangu ya afya ndiyo ilifanya jamaa zangu waone kuwa nitakuwa mzigo kwao, na hivyo wakaamua kunitelekeza,” akasema Bi Awuor.

Ni miaka miwili tangu Bi Awuor aanze maisha mapya katika nyumba hiyo ya wazee.

Hata hivyo, anasema kuwa upweke huwa unamkumba mara kwa mara, lakini mwishowe amekubali kuwa wanaoishi naye pale ndio familia yake mpya.

Bi Caroline Awuor akipimwa virusi vya corona na mhudumu wa afya kutoka kaunti ya Mombasa. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Jamaa zangu huwa hawaji hata kunisalimia. Wazee wanaoishi hapa na wafanyikazi wote ndio familia yangu mpya. Cha muhimu ni kuwa na afya bora,” akasema.

Bi Awuor anasema kuwa anajivunia afya njema na anaweza kupata dawa haraka, kwa kuwa wana hospitali katika makazi hayo.

“Ninapougua, huwa naenda katika hospitali yetu hapa na kuhudumiwa na daktari wetu. Chakula, malazi yote napata hapa na ninashukuru,” akasema.

Alikuwa anazungumza na Taifa Leo siku ambapo wazee katika makazi hayo walikuwa wanapimwa virusi vya corona, mnamo Agosti 13.

Bi Awuor alisema kuwa tangu Machi, baada ya kisa cha kwanza cha corona kutangazwa, hajaweza kutoka nje ya makazi hayo.

“Nimekuwa nikiskia katika redio na hata kuangalia katika televisheni kuwa kuna ugonjwa hatari wa corona. Pia, tumeambiwa tuvalie barakoa, tunawe mikono na tusikaribiane ili tujilinde na maradhi hayo,” akasimulia Bi Awuor huku akisema kuwa wanasubiri majibu ndipo waweze kujua kama wako salama ama wameambukizwa maradhi ya Covid-19.

Mhudumu wa jamii katika makazi ya wazee ya Alms, Bi Elvina Mzungu alisema kuwa kaunti ya Mombasa inagharamia mahitaji yote ya wazee hao kuanzia chakula, malazi hadi matibabu.

“Bi Awuor ameimarika kiafya na kwa muda ambao amekuwa hapa, ameweza kurejea hali yake ya kawaida. Pia kwa wenzake tunajaribu kuwahudumia kadri ya uwezo wetu. Zaidi, tunawaheshimu wazee hawa na hata wanapoaga dunia, huwa tunawaita viongozi wa dini waongoze ibada ya mazishi yao, kama binadamu yeyote yule wa kawaida,” akasema Bi Mzungu.

Baadhi ya wazee katika kituo cha Alms, Mombasa. PICHA/ DIANA MUTHEU

Alisema kuwa wanazingatia sheria ya kutoruhusu watu kujumuika na wazee hao, ili kuwakinga wasiambukizwe virusi vya corona.

“Tangu kesi ya kwanza ya corona itangazwe humu nchini, tuliwacha kuwakubalia watu kuingia ovyoovyo kituoni. Wazee wengi hapa wanashida tofauti za kiafya, wengine ni walemavu. Kwa hivyo ni jukumu letu kuwalinda na maradhi hayo,” alisema Bi Mzungu.

Mhudumu huyo wa jamii alisema kupima corona ni jambo muhimu kwa kuwa wazee hao na wahudumu wote katika kituo hicho, watapata kujua hali yao ya maradhi hayo.

“Japokuwa ni wakongwe, bado ni binadamu kama wengine. Wanapima ili wajue hali yao kama wananchi wale wengine,” akasema.