Habari MsetoSiasa

Masaibu yanayokwandama uliyasaka mwenyewe, Kabogo amwambia Waititu

May 29th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

ALIYEKUWA gavana wa Kiambu William Kabogo amemkashifu Gavana Ferdinand Waititu, akisema kuwa Bw Waititu amekuwa akitumia jina lake kujitakasa kutokana na masaibu yanayomkumba.

Bw Kabogo, ambaye ni hasimu mkubwa wa Gavana Waititu alisema kuwa hahusiani kwa vyovyote na uchunguzi ambao gavana huyo anafanyiwa, akimtaka kubeba mzigo wake mwenyewe.

Bw Kabogo, ambaye alichapisha ujumbe katika akaunti yake ya Facebook Jumatano alisema anaweza kumhurumia lakini hawezi kumsaidia Bw Waititu.

“Bw Waititu, wacha kutaja jina langu kila unapopata fursa katika vyombo vya habari. Sihusiani kwa vyovyote na uchunguzi ambao unafanyiwa, hayo ni majeraha ya kujiwekea,” akasema Bw Kabogo.

Gavana huyo wa zamani aliendelea, “Beba mzigo wako peke yako au na wale mliokula nao. Ninakuhurumia lakini siwezi kukusaidia, wacha kupiga kivuli ngumi.”