Habari za Kitaifa

Masaibu zaidi kwa raia ushuru ukiongezwa

May 12th, 2024 2 min read

NA WINNIE ONYANDO

WAKENYA wataendelea kuingia mfukoni zaidi wakati huu gharama ya maisha inaendelea kupanda, baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha pendekezo la Wizara ya Fedha ya kuongeza bei ya bidhaa za kimsingi kama vile mkate.

Hii ni ilifuatia Bunge la Kitaifa kuidhinisha pendekezo lililowasilishwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u ya kutaka kuanzishwa kwa ushuru wa VAT kwa mkate, maziwa na bidhaa nyingine.

Kando na mkate, bunge pia limepitisha pendekezo la kuanzisha ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kwa gharama ya huduma za kifedha kama vile kadi za kidijitali za kupokea mkopo na zile za kutoa pesa, kodi za kutuma pesa kupitia M-pesa, pombe aina ya Vodka na Whiskey na kodi inayolipwa kila mwaka na walio na gari.

Kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali, VAT ya kutuma pesa kupitia M-pesa, Sacco na benki imepanda kutoka asilimia 15 hadi asilimia 20.

Kwa upande mwingine, walio na magari sasa watalipa kati ya Sh5,000 na Sh100,000 kulingana na thamani ya gari.

“Bila kujali masharti mengine yoyote ya Sheria hii, ushuru wa magari utalipwa kwa Kamishna wa utoaji wa bima. Kodi ya gari italipwa kulingana na thamani ya gari, kwa kiwango kilichoainishwa hapo juu. Isipokuwa kwamba kiasi cha kodi kinacholipwa- hakitakuwa chini ya Sh5,000 na haitakuwa zaidi ya Sh100,000,” sehemu ya ripoti hiyo ilisoma.

Magari yakiwa kwa msongamano. PICHA | MAKTABA

Nayo bei ya mkate wa gramu 400 itapanda kwa angalau Sh10.

Kulingana na Prof Ndung’u, kuondolewa hatua ya serikali kusaza bidhaa kama vile mkate dhidi ya utozaji wa ushuru wa VAT imefaidi matajiri kwa kiwango kikubwa kuliko maskini.

Waziri huyo mnamo Machi alisema kuwa japo bidhaa kama vile mkate zinachukuliwa kuwa ni za watu wa tabaka la chini, serikali inaweza kufaidika pakubwa ikiwa itatoza ushuru wa juu.

“Tumegundua kuwa tunaweza kupata pesa nyingi kutoka kwa bidhaa hizo. Hii ndio maana kuna haja ya kuongeza VAT kwa mkate na bidhaa nyingine. Ukweli ni kwamba watu wa tabaka la chini ambao wanafaa kunufaika hawafaidiki,” Prof Njuguna alisema.

Kulingana na yeye, jumla ya VAT inayokusanywa nchini Kenya inajumuisha takriban asilimia 40 ya ushuru wote lakini asilimia 18 yake hurejeshwa kwenye bidhaa zinazodhaniwa kutumiwa na maskini.

Hata hivyo, waziri huyo alidai kuwa bidhaa hizo hutumiwa na watu wa tabaka la kati na kuongeza kuwa muundo wa sasa ambapo VAT kwa mkate haujabainishwa unawafanya watu wa tabaka la juu kuendelea kunufaika.

Mabadiliko haya kuhusu ushuru yanajiri huku mafuriko yakiendelea kuhangaisha Wakenya.

Baadhi ya wahasiriwa wa janga la mafuriko walipoteza wapendwa wao, mali na hata makazi.