Masaibu zaidi kwa Solskjaer baada ya Watford kupepeta Man-United ligini

Masaibu zaidi kwa Solskjaer baada ya Watford kupepeta Man-United ligini

Na MASHIRIKA

WATFORD walizidisha masaibu ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ugani Old Trafford kwa kuwapokeza Manchester United kichapo cha 4-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ugani Vicarage Road.

Masihara ya kiungo Scott McTominay yalichangia bao la kwanza ambalo Watford walifungiwa na Joshua King kabla ya Ismaila Sarr kufanya mambo kuwa 2-0 mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ingawa Donny van de Beek alirejesha Man-United mchezoni katika dakika ya 50, chombo cha mabingwa hao mara 20 wa EPL kilianza kuvuja katika dakika ya 69 baada ya beki Harry Maguire kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano na kufurushwa uwanjani.

Tukio hilo lilichochea Watford kukita kambi langoni mwa wageni wao na wakapata mabao mawili ya haraka mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia Joao Pedro na Emmanuel Dennis.

Kichapo ambacho Man-United walipokezwa kiliwasaza katika nafasi ya saba kwa alama 17 sawa na Brighton. Ni pengo la alama nne pekee ndilo linatamalaki kati ya Man-United na Watford inayoshikilia nafasi ya 16 chini ya mkufunzi Caludio Ranieri.

Matokeo duni ya Man-United sasa yanamweka Solskjaer katika presha ya kutimuliwa ugani Old Trafford huku vyombo vingi vya habari vikiripoti kwamba tayari Bodi ya Usimamizi imefikia maamuzi ya kumpiga kalamu.

Man-United wameshinda mechi moja pekee kutokana na saba zilizopita za EPL huku wakijizolea alama nne pekee kutokana na 21 ambazo walikuwa na uwezo wa kutia kapuni.

Brendan Rodgers wa Leicester City na kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane, ni baadhi ya wakufunzi wanaopigiwa upatu kutwaa mikoba ya Man-United iwapo kikosi hicho kitaagana rasmi na Solskjaer.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Majibizano hatari kwa Ruto Mlimani

3 walazwa hospitalini Marsabit baada ya kushambuliwa

T L