Habari

Maseneta Kenya wafahamishwa wafungwa 1,700 wamepatikana na Covid-19

October 23rd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JUMLA wa wafungwa 1,700 wamepata maambukizi ya virusi vya corona tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini mnamo Machi 13, 2020, Mkurugenzi wa Huduma za Afya Jackton Kisivuli amesema.

Afisa huyo ameongeza kuwa kufikia sasa jumla ya wafungwa watatu wamefariki kutokana na homa hiyo hatari.

Dkt Kisivuli amefichua hayo wakati wa mkutano ulioleta pamoja Kamati ya Seneti kuhusu Afya, Wizara ya Masuala ya Ndani na Idara ya Magereza. Mkutano huo umeendeshwa kwa njia ya mtandao kutumia programu ya Zoom.

“Kutokana na hatari ya wafungwa kuambukizwa corona kutokana na msongamano, Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Wizara ya Masuala ya Ndani zimehimiza kwamba wafungwa wenye makosa madogo waachiliwe huru,” akasema Dkt Kisivuli.

Kamishna Mkuu wa Idara ya Magereza Wycliffe Ogalo amesema ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona katika magereza linatokana na ugumu wa kuzingatia kanuni ya mtu mmoja kukaa umbali wa si chini ya mita moja kutoka kwa mwenzake.

“Hata hivyo, ningependa kuwapongeza maafisa wa magereza na wafungwa kwa kujizatiti kufuata masharti mengine ya kuzuia maambukizi ya corona katika mazingira magumu,” akasema.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Masuala ya Ndani Hussein Dado amesema magereza nchini yamejengwa kuwa na uwezo wa kusitiri hadi wafungwa 30,000 pekee.

“Lakini tunashuhudia shida ya msongamano kwa sababu wakati huu kuna jumla ya wafungwa 55,000 katika taasisi hizo. Tunapongeza Idara ya Mahakama kwa kuingilia kati na kuwaachilia wafungwa wenye makosa madogomadogo. Kwa hivyo, sasa idadi ya wafungwa imeshuka hadi 46,000 ambayo ingali juu,” akasema Bw Dado.

Waziri huyo msaidizi amesema wizara yake imechukua hatua na kufaulu kuwatenga wagonjwa walioambukizwa corona katika gereza la Nairobi, lililoko eneo la Viwandani.

Mkutano huo uliambiwa kuwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi, kamati maalum imeundwa ya kusimamia mikakati hiyo.

Kamati hiyo yenye wanachama kutoka vitengo mbalimbali katika idara ya magereza itakuwa ikitoa ripoti kila wiki kwa Kamishna Mkuu wa Magereza Bw Ogalo.

“Kando na hayo wafungwa wote wapya watakuwa wakiwekwa karantini kwa siku 14 kabla ya kuruhusiwa kujumuika na wafungwa wengine,” akasema Bw Ogalo.

Mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kuangazia mikakati ambayo serikali imeweka kudhibiti maambukizi ya Covid-19 katika magareza ya humu nchini.

Hii ni baada ya Seneta Maalum Falhada Dekow kuitisha taarifa kutoka kwa Wizara husika kuhusu hali ya maambukizi ya Covid-19 katika magereza ya Kenya.