Maseneta mbioni kupitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Maseneta mbioni kupitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti litafanya kikao maalum Jumanne kujadili Mswada wa marekebisho ya Sheria ya Matumizi ya Dawa za Kusisimua Misuli miongoni mwa wanariadha (Anti-Doping Amendment Bill 2020).

Kikao hicho, ambacho kitafanyika katika ukumbi wa seneti saa nane na nusu alasiri, kitafanyika kwa njia ya maseneta kuhudhuria moja kwa moja na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Mswada huo ambao ulipitishwa katika bunge la kitaifa wiki jana, unalenga kufanikisha utendakazi wa shirika la kupambana na matumizi ya dawa katika spoti (Anti-Doping Agency of Kenya) nchini, haswa riadha.

Utafanya hivyo kwa kuoanisha Sheria ya Kupambana na Dawa za Kusisimua Misuli 2016 na Kanuni za 2021 za Kupambana na Dawa Hizo Ulimwenguni. Kenya ni mojawapo ya mataifa yaliyotia saini mkataba wa kuzingatia kanuni hizo.

Kupitishwa kwa mswada huo kutawezesha Kenya kutimiza kanuni za kimataifa kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

“Hii itawasaidia wanariadha wa Kenya kuendelea kushiriki katika mashindano ya riadha humu nchini, kanda, barani Afrika na yale ya ulimwenguni na kutambua umuhimu wa kuzuia matumizi ya dawa zilizoharamishwa katika sporti,” unasema mswada huo.

Akishiriki mjadala kuhusu mswada huo katika bunge la kitaifa wiki jana, mwenyekiti wa kamati ya michezo katika bunge hilo Patrick Makau alisema hivi: “Huu mswada ni muhimu zaidi kwa taifa hili kwani utahakikisha kuwa Kenya inatimiza kanuni za Shirika la Kimataifa la Kupambana na matumizi ya Dawa zilizoharamishwa Michezo (World Anti-Doping Agency-WADA) na lile la Kupambana na Matumizi ya Dawa hizo Kenya (Anti-Doping Agency of Kenya-ADAK).

Kamati hiyo inayoongozwa na Bw Makau (ambaye ni Mbunge wa Mavoko) ndiyo ilishughulikia mswada huo katika bunge la kitaifa.

Kenya ni taifa linalotambuliwa na kusifiwa kwa kuwa na wanariadha wenye talanta za kipekee haswa katika mbio za masafa marefu. Ushindi wao katika mashindano ya kimataifa umeiletea Kenya sifa na heshima katika mida ya kimataifa.

Hata hivyo, ongezeko la visa vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu zilizoharamishwa miongoni mwa wanariadha wa Kenya katika miaka michache iliyopita imeiletea Kenya sifa mbaya katika fani hiyo ya spoti.

Tayari zaidi ya wanariadha 50 wa Kenya, miongoni mwao wakiwa ni wale waliong’aa katika mashandano ya Olimpiki kama vile Asbel Kiprop na Jemimah Sumgong, wamepigwa marufuku kushiriki mashindani ya riadha humu nchini na ulimwenguni kwa vipindi tofauti kwa kupatikana wametumia dawa hizo.

Kiprop alishinda mbio ya mita 1,500 katika mashindano ya Olimpiki ya 2008 huku Sumgong akishinda katika mbio za marathon katika Olimpiki ya 2016.

Wengine waliopigwa marufuku kwa kupatikana wametumia dawa ni Mshindi wa Dunia katika mbio za mita 1,500 mnamo 2017 Elijah Managoi, aliyekuwa Bingwa wa Dunia katika Mbio za Marathon Wilson Kipsang, Daniel Wanjiru (aliyekuwa Bingwa wa London Marathon) na Rita Jeptoo ambaye ni Bingwa wa zamani wa Bostona na Chicago Marathon kwa Wanawake.

Inalazimu kwamba Maseneta wapitishe mswada huu kabla ya Desemba 31, 2020 ili usipitwe na wakati na kupelekea Kenya kufungiwa nje kushiriki katika mashindano ya riadha ya kimataifa.

Kenya ilitia saini Mkataba wa Unesco unaopinga matumizi ya dawa katika spoti mnamo 2009. Kwa hivyo, ilikuwa mojawapo ya mataifa wanachama wa mkataba huo na unashurutishwa kutekeleza kanuni ya kimataifa kuhusu vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo zilizoharamishwa.

Kanuni mpya kuhusu vita dhidi ya uovu huu itaanza kutekelezwa mnamo Januari 1, 2021 ambayo imeanzisha viwango vipya katika mapambani dhidi ya matumizi ya dawa hizo.

You can share this post!

Wanafunzi wengi zaidi kusomea chini ya miti 2021

SAMMY WAWERU: Nairobi inahitaji gavana atakayeiletea hadhi...