Habari

Maseneta roboti

December 19th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KURA ya kumtimua Gavana Mike Sonko wa Nairobi mnamo Alhamisi usiku imewaangazia maseneta kama mateka wa vigogo wakuu wa siasa nchini.

Kulingana na matokeo ya kura hiyo, maseneta wanaoegemea handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga walipiga kura ya ‘Ndio” kumng’oa Bw Sonko madarakani, huku wale wa mrengo wa ‘Tangatanga’ unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto wakipiga kura ya ‘La’.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa maseneta hao walikuwa wameshaafikia uamuzi kulingana na mirengo wanayoegemea hata kabla ya vikao vya siku mbili kujadili mswada wa kumwondoa Bw Sonko.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika Seneti aliambia Taifa Leo kwamba maseneta wa mirengo yote miwili walikuwa tayari wamepata amri kutoka kwa “wakubwa wao” wapige kura jinsi walivyofanya.

“Tangu hoja hiyo ilipoanza kujadiliwa, tayari kila moja ya kambi mbili katika Seneti ilikuwa imechukua msimamo wake. Wandani wa Uhuru na Raila walikuwa wameagizwa kuidhinisha mashtaka yote huku wenzao wa Tangatanga wakitwikwa kazi ya kumnusuru Bw Sonko kwa kupinga madai dhidi yake,” akasema afisa mmoja wa cheo cha juu katika Seneti.

Wakili Ambrose Weda alitoa kauli kama hiyo akitaja kikao cha kujadili mswada wa kutimua Bw Sonko kama cha kupoteza wakati na fedha za umma ilihali hatima ilikuwa tayari imeamuliwa kwingine.

“Mawakili wa bunge la Kaunti ya Nairobi wasifurahie ushindi wowote. Maseneta hawakufanya maamuzi yao kwa misingi ya hoja. La hasha! Maseneta hao 27 walikuwa vikaragosi au maroboti ya wakuu wao ambao ndio walitaka Bw Sonko aondolewe,” akasema Bw Weda kwenye mahojiano na Taifa Leo jana Ijumaa.

“Wanaoshikilia mamlaka ya nchi walikuwa wamechoshwa na ukaidi wa Sonko haswa baada ya kuinyima Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) fedha za matumizi kwa kudinda kutia saini bajeti ya serikali ya kaunti,” Bw Weda ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya siasa akaongeza.

Kabla ya upigaji kura kuanza, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala aliwaambia mawakili wa Bw Sonko kwamba uzingatiaji wa sheria haungemnusuru Bw Sonko.

“Kile ambacho hupewa kipaumbele katika mchakato kama huu wa kumwondoa gavana afisini ni siasa wala sio sheria. Tusipoteze muda. Tumefikia uamuzi na unukuu wa sheria mbalimbali hautabadili msimamo wetu,” Bw Malala akamwambia wakili wa Sonko, Wilfred Nyamu.

Hatua hiyo imetoa picha ya kusikitisha kuwa maseneta ni kama maroboti yasiyo na uwezo wa kufanya maamuzi kwa kutumia busara hoja na sheria.

Maseneta 27 wa mrengo wa handisheki walipiga kura ya ‘Ndio’ na kuidhinisha mashtaka yote dhidi ya Bw Sonko yaliyokuwa kwenye hoja iliyopitishwa na bunge la kaunti ya hiyo mnamo Desemba 3.

Nao maseneta 16 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walipiga kura ya ‘La’ huku nao Johnson Sakaja (Nairobi) na Mutula Kilonzo Junior (Makueni) wakisusia upigaji kura.

Naye Seneta wa Garissa Yusuf Haji hakuwepo kwa sababu anaugua ilhali Seneta wa Machakos Boniface Kabaka alifariki juzi.

Kikosi cha handisheki, ambacho uaminifu wake ni kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga kiliongozwa na Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio, Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata na Kiongozi wa Wachache James Orengo.

Maseneta wa Tangatanga ambao ni watiifu kwa Dkt Ruto nao waliongozwa na Kipchumba Murkomen.