Maseneta sita wa Jubilee watimuliwa kwa ukaidi

Maseneta sita wa Jubilee watimuliwa kwa ukaidi

Na CHARLES WASONGA

MASENETA Isaac Mwaura na Millicent Omanga ni miongoni mwa maseneta sita maalum ambao wametimuliwa kutoka chama cha Jubilee kwa ukaidi wa sera na misimamo yake.

Kwenye taarifa Jumatatu jioni, Katibu Mkuu Raphael Tuju, amesema kuwa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) ilifanya kikao na kufikia uamuzi huo.

Wengine waliofurushwa ni maseneta Mary Seneta, Naomi Waqo, Victor Prengei na Imani Falhada Dekwa ambaye ni naibu kiranja wa wengi katika seneti.

“NMC kwa kutekeleza wajibu wake kulingana na kipengele cha 7 (2a) cha katiba ya chama, imeamuru kufurushwa kwa maseneta wafuatao: Isaac Mwaura, Seneta Mary Yiane, Waqo Naomi Jilo, Omanga Millicent, Prengei Victor, na Iman Dekow,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Bw Tuju.

Taarifa hiyo hata hivyo imesema kuwa uamuzi huo unaanza kutekelezwa mara moja lakini maseneta hao wako na mwanya wa kukata rufaa.

“Uamuzi wa NMC unaanza kutekelezwa mara moja na bunge la seneti na afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa zimejulishwa,” akaeleza Bw Tuju.

Wiki jana, Bw Mwaura alifika mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Jubilee kuhojiwa kuhusu madai ya kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta anayodaiwa kutoa Desemba 2020 katika mkutano wa kusherehekea ushindi wa Mbunge wa Msambweni Feisal Bader.

Na maseneta hao wengine watano walihojiwa na kamati hiyo Mei 2020 kwa kukaidi mwaliko wa mkutano wa Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi. Mkutano huo ulihudhuriwa na maseneta 20 wa Jubilee na Kanu.

You can share this post!

Majaji watano wazima IEBC kupeleka mswada wa BBI kwa kaunti...

Leteni hoja hiyo tupambane nayo, Tangatanga waambia Savula...