Habari

Maseneta tishio kwa ugatuzi

September 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

LEO Jumanne inakuwa mara ya 11 ambapo maseneta watajaribu kuamua utaratibu utakaotumika katika ugavi wa rasilimali kwa kaunti.

Na katika hali ambayo huenda ikafifisha zaidi ushawishi wa Bunge la Seneti, wadadisi na raia wa kawaida wasema maseneta sasa wamekwamisha utoaji huduma kutokana na vuta nikuvute ya muda mrefu.

Duru zilisema wanachama wa kamati maalum iliyotwikwa wajibu wa kusaka muafaka kuhusu suala hilo hawajakubaliana kuhusu mfumo bora wa kugawa Sh316.5 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika bajeti ya mwaka huu.

Viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM wamelaumu maseneta kwa kukataa kuelewana kwani inahofiwa hali hiyo itachelewesha zaidi usambazaji wa fedha kwa kaunti zote 47.

Tayari, kaunti mbalimbali zimelalamika kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi kwa miezi miwili tangu Julai kwa sababu ya mgogoro huo.

Katika hotuba za awali, Rais Kenyatta na Bw Odinga waliashiria uwezekano kuwa maseneta wanapigania masuala ya kibinafsi wala mzozo huo hauhusu hitaji la usawa wanavyodai.

“Ukiona kama kuna seneta ambaye watu wake wanatengewa pesa nyingi ilhali anapinga, sio eti anajali wale wengine zaidi. Hapo kuna nuksi. Kuna swali unafaa ujiulize… Hilo swali linataka jibu na litatoka kwao sio kwangu,” Bw Odinga alisema Jumapili alipozuru Kaunti ya Kakamega.

Seneta wa kaunti hiyo, Bw Cleophas Malala ni miongoni mwa maseneta waliopinga mfumo uliowasilishwa katika Seneti licha ya kuwa Kaunti ya Kakamega ni miongoni mwa zitakazofaidi.

Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa Chama cha ANC Musalia Mudavadi na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa pia ni miongoni mwa viongozi waliowataka maseneta wasuluhishe utata kuhusu ugavo huo.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya alitisha kwamba, kaunti zitasimamisha shughuli kuanzia Septemba 17 ikiwa kufikia wakati huo maseneta hawatakuwa wameelewana.

Baraza hilo pia limetisha kuanzisha mchakato wa kufutuliwa mbali kwa seneti ikiwa suala hilo halitasuluhishwa haraka.

“Tunaonya Seneti kwamba, ombi la kufutiliwa kwake linaweza kuwasilishwa na mwananchi yeyote kupitia Mahakama Kuu kulingana na kipengele cha 258 cha Katiba,” mwenyekiti huyo ambaye ni gavana wa Kakamega, akaonya.

Wafanyakazi wa serikali za kaunti, wakiwemo wahudumu wa afya wanaotekeleza wajibu muhimu wakati huu wa janga la corona, wamekosa mishahara tangu Juni ilhali maseneta wameshindwa kutatua utata kuhusu mfumo huo katika vikao tisa walioandaa.

Kupitishwa kwa mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa kaunti ndio utatoa nafasi ya kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti wa 2020. Baadaye, Msimamizi wa Bajeti (CoB) ataidhinishwa kusambazwa kwa kaunti, kwa awamu.

Wiki iliyopita, kamati hiyo maalumu, inayoongozwa kwa pamoja na maseneta Moses Wetang’ula (Bungoma) na Johnson Sakaja (Nairobi) ilitangaza kuwa imewasilisha ripoti yake kwa uongozi wa seneti huku ikielezea matumaini kuwa mvutano huo utaisha.

Hata hivyo, Taifa Leo imebaini kuwa iliwasilisha ripoti mbili, kinzani, kwa uongozi wa Seneti.

Ripoti yao ina mapendekezo mawili. Pendekezo la kwanza linaakisi mfumo uliopendekezwa na Seneta wa Meru Mithika Linturi ambayo inapandekeza kuwa Sh270 bilioni zigawanywe kwa kuzingatia mfumo wa zamani huku Sh46.5 bilioni zigawanywe kwa mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha.

Chini ya mfumo huo unaozingatia wingi wa watu, kaunti 28 zitapata nyongeza ya fedha huku 19 zikipoteza jumla ya Sh17 bilioni.

Pendekezo la pili linaakisi mapendekezo ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kirinyaga Charles Kibiru, na inapendekeza kaunti zenye idadi ya juu ya watu kuongezewa mgao wa fedha. Pendekezo hilo limepingwa na maseneta kutoka kaunti zitakazopoteza fedha.

Hata hivyo, Spika wa Seneti Ken Lusaka kwa mara nyingine ameelezea matumaini kuwa bunge hilo litatanzua mvutano kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti kesho.

Akiongea Bungoma Jumamosi, wakati wa mazishi ya kakake aliyekuwa Mbunge wa Kanduyi Alfred Khangati, Lusaka alisema Seneti itafanya kila iwezalo kuhakikisha kaunti zinapasa fedha.