Maseneta wa Azimio wamkosoa Ruto kuhusu GMO

Maseneta wa Azimio wamkosoa Ruto kuhusu GMO

NA MARY WANGARI

MASENETA wanaogemea muungano wa Azimio One Kenya wamekosoa hatua ya Rais William Ruto ya kuruhusu nchini vyakula vinavyokuzwa kisayansi (GMO).

Akihutubia baraza la mawaziri mnamo Jumatatu, Kiongozi wa Taifa aliondoa marufuku iliyotangazwa 2012 dhidi ya ukuzaji na uagiziaji wa vyakula vya GMO nchini.

Hatua hiyo illifanya Kenya kuwa taifa la pili baada ya Afrika Kusini kuidhinisha vyakula vilivyokuzwa kisayansi Barani Afrika.

Hata hivyo, wakizungumza Jumatano katika kikao cha Bunge la Seneti kilichoongozwa na Naibu Spika wa Seneti Kathuri Murungi, waunda sheria wanaomuunga mkono Raila Odinga walimshutumu Rais Ruto kwa kuhatarisha afya ya Wakenya kwa kisingizio cha kukabiliana na baa la njaa.

“Badala ya kuinua biashara za mahasla nchini, anaruhusu mashirika ya kigeni kujinufaisha kwa kuwekeza nchini na kuwapa sumu watu wetu kwa kisingizio cha kukabiliana na janga la njaa nchini. GMO inasababisha saratani,” alilalamika Seneta wa Nyamira Erick Omogeni.

Naibu Spika, hata hivyo, alimwagiza Seneta Omogeni kuwasilisha ripoti yenye ushahidi kuthibitisha madai yake yanayohusisha vyakula vya GMO na saratani.

Aidha, wanasiasa hao wakiongozwa na Seneta wa Narok Ledama Olekina, wametilia shaka kujitolea kwa Dkt Ruto katika kuimarisha demokrasia na kuangamiza ufisadi nchini.

Walilalamikia kile walichotaja kama njama za Rais Ruto za kusambaratisha upinzani kwa kuvizia viongozi waliochaguliwa kupitia vyama vya muungano wa Azimio unaoongozwa na Bw Odinga.

“Tunataka Rais atimize kauli yake kuhusu kudumisha demokrasia na upinzani imara utakaoangazia utendakazi wa serikali. Tumemwona Rais akiwavizia na kuwateka wanachama kutoka ng’ambo hiyo nyingine na kujihusisha na uundaji wa miungano kinyume na sheria,” alihoji Seneta Olekina.

Kwa upande wake, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alikosoa mikakati ya Dkt Ruto ya kuangamiza ufisadi huku akimlaumu kwa kukosa kuangazia suala hilo kikamilifu alipohutubia Baraza la Mawaziri Jumatatu.

Huku akielezea wasiwasi wake kuhusu Hazina Mpya ya Mahasla pamoja na mageuzi yaliyotangazwa na Rais Ruto kuhusu Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) alipendekeza kubuniwa kwa sheria na sera thabiti ili kuzuia hazina hizo kugeuzwa vituo vya kuendeleza ufisadi.

“Hatuwezi kusema tunataka kuweka pesa zaidi katika NSSF bila kuifanyia marekebisho. Hakikisha NSSF imerekebishwa ili Wakenya wawe na imani ya kuweka pesa zao katika hazina hiyo,” alihoji.

“Hazina ya Mahasla itakuwa kituo kingine cha ufisadi ikiwa sheria mwafaka hazitawekwa. Ni sharti kuwepo thamani ya pesa na uwajibikaji ufaao,” alisema.

“Nimetamaushwa kwamba rais hakuzungumza kuhusu ufisadi. Tulitarajiwa kwamba angetueleza kuwa moja kati ya njia za kupata pesa ni kwa kukomesha ufisadi. Tunashangaa ni vipi rais atatekeleza miradi hii yote bila kukomesha ufisadi,” alisema.

Gharama ya juu ya maisha pamoja na ujumuishaji wa jamii na maeneo yaliyotengwa kwenye orodha ya baraza jipya la mawaziri lililotangazwa na Dkt Ruto Jumatatu ni suala lingine lililoibua hisia mseto katika Bunge la Seneti.

“Sijaona mama mboga yeyote wala mchuuzi katika baraza hilo. Badala yake rais anawatuza wandani wake. Bei za unga bado ziko juu,” alihoji Seneta Osotsi.

Seneta wa Tana River, Danson Mungatana alihimiza serikali kutekeleza mipango yake kuhusu usambazaji wa raslimali ili kusaidia jamii zilizotengwa.

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Uanahabari katika shule ya upili ya...

IEBC yatangaza chaguzi ndogo Bungoma na wadi tano nchini

T L