Habari

Maseneta wafokea mswada unaolenga kuzima azima yao kuwa magavana

Na COLLINS OMULO July 3rd, 2024 2 min read

MSWADA unaolenga kuwazuia magavana wa zamani kugombea udiwani au useneta baada ya kukamilisha mihula miwili, inaelekea kukataliwa na maseneta kutokana na azma za kisiasa.

Haya yanajiri huku kukiwa na upinzani mkali kutoka kwa maseneta wanaomezea mate ugavana huku wakigawanyika kuhusu Mswada huo.

Mswada huo unalenga kuwazuia watu ambao wamehudumu kama magavana, kuwania kama maseneta au madiwani kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kukamilisha hatamu zao.

Hata hivyo, sheria hiyo iliyopendekezwa na Seneta Mteule, Raphael Chimera, imepingwa vikali na idadi kubwa ya maseneta, wanaohoji kuwa itazima haki na uhuru wao kisiasa, ikiwa itapitishwa.

Maseneta Samson Cherargei (Nandi) Godfrey Osotsi (Vihiga) na mwenzao wa Kiambu, Karungo Thang’wa, wamekuwa mstari wa mbele kupinga Mswada huo.

Watatu hao wanamezea mate viti vya ugavana katika kaunti zao mtawalia.

Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, licha ya azma yake kuwania afisi ya mkuu wa Kaunti hiyo, anapanga kustaafu ikiwa atanyakua kiti hicho.

Seneta Chimera anahoji kuwa Mswada huo unadhamiriwa kuruhusu kukamilisha michakato fulani inayoendelea kuhusu uwajibikaji, kama vile ukaguzi wa hesabu za serikali za kaunti.

Alisema matokeo ya michakato hiyo, itatoa mwongozo kuhusu iwapo mhusika anastahili kuongoza afisi nyingine ya kuchaguliwa.

Seneta huyo anaeleza kuwa magavana wa kaunti, wakati wa hatamu zao, wanahitajika kuwajibikia bunge za kaunti na Seneti kuhusu maamuzi yoyote wanayofanya kifedha na kiusimamizi.

Hata hivyo, Seneta Cherargei, akipinga Mswada huo ulipojadiliwa Seneti, alihoji kuwa, unakiuka Kifungu 38 cha Katiba, kuhusu haki na uhuru wa kisiasa kwa sababu unanuia kumzuia, kwa njia isiyo ya haki, mtu yeyote kugombea kiti cha uchaguzi.

Alisema japo Mswada huo una nia njema, unahujumu uhuru na haki Kifungu 24 cha Katiba kinavyoeleza na pia unazima ushindani wa kisiasa.

“Tunatibu dalili badala ya maradhi. Upeo wa demokrasia ulimwenguni kote umewekwa wazi. Kama magavana wanataka kuwania useneta, acha iwe hivyo” alisema Bw Cherargei.

Bw Chimera alihoji kuwa pendekezo hilo linalolenga kuwazuia magavana kuwania useneta na udiwani lina mantiki na ni la haki kwa sababu linalenga afisi zinazotekeleza moja kwa moja uangalizi wa serikali za kaunti.

Alisema kipindi cha miaka mitano ya “mapumziko” kitaruhusu Seneti na bunge za kaunti, kuwa na muda wa kuchunguza masuala yanayozuka kuhusu ukaguzi wa hesabu za kaunti husika kwa namna isiyo na mapendeleo wala kuhofia kuwa mhusika anayepaswa kujibu maswali hayo ni kiongozi mwenzao.