Siasa

Maseneta wakana dai la kuwapunja magavana

September 5th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC), imekana madai kuwa wanachama wake huwapunja magavana wanapofika mbele yake kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha katika kaunti zao.

Kwenye kikao na wanahahabari katika majengo ya bunge jana, mwenyekiti wa kamati hiyo Sam Ongeri alisema madai hayo yaliyotolewa na baraza la magavana ni njama ya wao kutaka kukwepa kuwajibikia usimamizi wa mabilioni ya fedha za umma.

“Madai hayo hayana msingi wowote. Tutaendelea kuwaalika wawajibikie fedha za umma. Hatufanya mikutano ya mtandaoni wanavyopendekeza, wakitaja uwepo wa ugonjwa hatari wa Covid-19,” akasema.

Prof Ongeri aliongeza kuwa kipengele cha 125 cha Katiba kinaipa Seneti na kamati zake mamlaka ya kuwaagiza maafisa wa umma, wakiwemo magavana, kuwajibikia matumizi ya rasimali za umma wanazosimamia.

“Uwajibikaji huo ni wa kibinafsi wala sio wa pamoja,” akasema.

Alikuwa ameandamana na maseneta; Irungu Kang’ata (Murang’a), Samson Cherargei (Nandi), Johnnes Mwaruma (Taita Taveta) na Ochilo Ayacko (Migori).

Prof Ongeri alisisitiza kuwa Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria sharti afike mbele ya kamati yake Septemba 10 alivyoagizwa baada ya kudinda kufika mnamo Agosti 28.

Hiyo ilikuwa ni mara ya tatu ndani ya kipindi cha miezi miwili kwa Bw Wa Iria kukosa kufika mbele ya CPAIC.

Kamati hiyo ilimtoza faini ya Sh500,000 na kumwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai amkamate na kumwasilisha katika kikao hicho.