Maseneta wakemea wanahabari kwa kuchapisha video waliyodai ni ya Kang’ata akiwa mlevi

Maseneta wakemea wanahabari kwa kuchapisha video waliyodai ni ya Kang’ata akiwa mlevi

Na CHARLES WASONGA

MASENETA Jumatano walishambulia vyombo vya habari kufuatia video feki iliyosambazwa mitandaoni iliyokosea heshima mwenzao, Seneta wa Murang’a Irung’u Kang’ata.

Hii ni baada ya Bw Kang’ata kulalamikia hatua ya Citizen Digital, Kameme FM, K24 TV na The Star kuweka video moja iliyomsawiri Bw Kang’ata kama aliyekuwa akishiriki shughuli za Seneti akiwa mlevi kwenye baa ya Sabina Joy, Nairobi.

“Mheshimiwa nakata uwaamuru wahariri wa vyombo hivi vya habari wafike mbele ya Kamati ya Mamlaka na Hadhi ya Seneti ili waeleze ni kwa nini walisambaza video feki ya kuniharibia jina. Video hiyo pia iliharibu hadhi ya bunge hili na maseneta hawa waheshimiwa,” akalalama.

Bw Kang’ata alidai kuwa kinyume na taswira na sauti katika video hiyo, hajawahi kunywa pombe wala kuvuta sigara maishani mwake.

“Hakuna tone la pombe limewahi kupita kinywani mwangu. Sauti kwenye video inayosambazwa ilivurugwa na wanablogu wa Kieleweke ili kunipaka tope kisiasa,” akasisitiza.

Maseneta wenye hasira walitumia mwanya huo kukaripia vyombo vya habari kwa ujumla kutokana na kile walichodai ni mienendo ya kusambaza habari za kupotosha kuhusu matukio katika Seneti.

Bw Enock Wambua (Kitui), ambaye alikuwa mwanahabari kabla ya kuingia siasa, Moses Watang’ula (Bungoma), Abdullahi Ali (Wajir) na Aaron Cheruiyot (Kericho) walipendekeza kuwa vyombo hivyo vizimwe kuripoti shughuli za Seneti.

“Kama mwanahabari mwenye tajriba ya miaka mingi, najua kuwa vyombo vya habari vinapasa kuongozwa na maadili ya uanahabari. Wale waliosambaza video hiyo chafu wamekiuka maadili hitajika na wanafaa kuadhibiwa,” akasema Bw Wambua.

Naye Bw Cheruiyot alipendekeza kuwa wakuu wa vyombo hivyo wafike pia mbele ya Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwani ndio yenye uwezo wa kuchunguza uovu kama huo ambao alitaja kama “dhuluma ya kimtandaoni”.

Baada ya mjadala mkali Spika Lusaka alisema kuwa atachunguza video hiyo iliyodaiwa kuwa feki na kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo Jumanne wiki ijayo.

Hata hivyo, Jumatano jioni K24 TV na gazeti la The Star zilimwomba msamaha Seneta Kang’ata kutokana na aibu ambayo video hiyo ilimsababishia.

“Tunaomba msamaha kwa video iliyowekwa katika mtandao wetu iliyodai kuwa Seneta Irungu Kang’ata aliingia, kieletroniki, katika kikao cha Seneti akiwa ndani ya klabu ya Sabina Joy. Tumegundua kuwa video hiyo ilivurugwa,” ikasema The kwenye taarifa katika akaunti yake ya Twitter.

“Tunaomba msamaha kwa video moja iliyowekwa katika mtandao wetu iliyodai kuwa Seneta Irungu Kang’ata alijiunga na kikao cha seneti kutoka Sabina Joy. Tumegundua kuwa sauti kwenye video hiyo ilikuwa feki ambayo iliwekwa juu ya video halali,” ikasema K24 TV huku ikiweka video halisi ya shughuli za Seneti Jumanne.

Seneta huyo aliwahi kuhudumu kama kiranja wa wengi katika Seneti kabla ya kufurushwa mnamo Juni mwaka huu kwa madai kumdharau Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee.

Wakati huu anapania kuwania Ugavana wa Murang’a kwa kutumia tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

You can share this post!

Gavana Waiguru, Kibicho wazika uhasama

Mkulima hodari anavyotengeneza mbolea asilia