Habari Mseto

Maseneta wakosoa ujenzi wa daraja la watu pekee kivukoni

September 3rd, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

KAMATI ya seneti inayoshughulikia masuala ya janga la corona, imekosoa ujenzi wa daraja la watu pekee unaoendelea katika kivuko cha Likoni.

Naibu mwenyekiti ya kamati hiyo, Bw Mithika Linturi, alisema mradi huo ulifaa kuwahusisha wakazi ili kupata maoni yao kabla ya kuanza ujenzi huo.

“Huu ni mradi mkubwa. Hatutaki daraja lililogharimu Sh1.7 bilioni kuja kuhatarisha maisha ya wakazi,” akasema.

Alitaka kujua iwapo daraja hilo litatumia umeme kuhudumu. “Kama tunavyojua nchini kuna changamoto ya umeme, je jambo hili limeangaziwa vilivyo? Hatutaki itokee hali ya kuwa meli inakuja kisha umeme upotee,” akasema.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bw Bakari Goa alisema daraja hilo halitatumia umeme bali litaunganishwa na meli mbili za kuvuta ambazo ndizo zitaliwezesha kufunga na kufungua.

Seneta wa Mombasa, Bw Mohammed Faki alitaka kujua kama shirika hilo limeweka njia mbadala endapo mashine hizo zitakwama wakati meli inaingia.

Bw Gowa alisema kuwa shirika lake halikuhusika na kupendekeza ujenzi wa daraja hilo, bali wazo hilo lilitoka kwa serikali ya kitaifa.

“Tuliletewa mswada huu na tukaelezwa kuwa daraja litasaidia kupunguza msongamano ambao umekuwa ukishuhudiwa katika eneo hili. Shirika la Kenya Ferry lilishiriki tu katika kupendekeza sehemu daraja hilo litakapo jengwa,” akasema.

Daraja hilo linatarajiwa kukamilika kufikia mwishoni mwa mwaka.Katika kutekeleza masharti ya kujikinga dhidi ya virusi vya corona, Bw Goa alisema wamehakikisha kuwa wakazi wanaotumia kivuko hicho wanavalia maski kabla ya kuabiri feri.

Aidha alisema wameweka mifereji 100 kwa kila ngambo kuhakikisha wanaotumia kivuko hicho wanaosha mikono na sabuni kabla ya kuabiri feri.

Pia waliomba serikali kuwasaidia kukarabati vibanda vya kunyunyizia watu dawa za kuuwa viini wakisema vilivyoko vimeharibika.

Kamati ya seneti iko katika ziara ya kaunti za Pwani kuangalia masuala mbali mbali yakiwemo kukiukwa kwa haki za kibinadamu tangu kuzuka kwa janga la corona na ufujaji wa pesa.