Habari

Maseneta wamtaka Rais kubuni jopokazi kuchunguza madhila ya sekta ya chai

October 9th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kubuni jopokazi la kuchunguza changamoto zinazoisibu sekta ya majanichai nchini; hali ambayo imesababisha kushuka kwa mapato ya wakulima kupitia malipo duni ya bonasi mwaka huu wa 2019.

Viongozi hao pia wanataka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuwachunguza wasimamizi wa Mamlaka ya Ustawi wa Kilimo cha Majanichai Nchini (KTDA) kwa kile walichodai ni usimamizi mbaya wa pesa za wakulima wa zao hilo.

“Tunataka jopokazi hili kubuniwa ili lichunguze kiini cha shida ambazo wakulima wa majanichai wanapitia na kutoa mapendekezo kwa Rais Kenyatta kuhusu njia za kuboresha kilimo hicho. Serikali haiwezi kuketi na kutizama huku sekta hii inayotegemewa na zaidi ya wakulima milioni moja wakiendelea kuteseka,” akasema Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano.

Kiongozi huyo ambaye anawakilisha eneo kunakokuzwa majanichai kwa wingi alikuwa ameandamana na mwenzake wa Nyeri Ephraim Maina.

Bw Cheruiyot alisema ombi hilo la maseneta lilitarajiwa kuwasilishwa Jumanne alasiri katika Ikulu ya Rais na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka akiandamana na karani wa bunge hilo Jeremiah Nyengenye.

“Wakulima wa majanichai nchini hawawezi kuishi maisha ya ufukara ilhali sekta hiyo huzalisha mapato ya zaidi ya Sh100 bilioni kila mwaka kutokana na usimamizi mbaya wa sekta hii. Huu unyanyasaji wa wakulima unapasa kukoma mara moja,” akasema.

Mwaka huu wakilima wa majani chai walilipwa bonasi ya Sh17 kwa kilo, kwa wastani, ilhali mwaka jana walipokea malipo ya Sh58 kwa wastani.

Hii imesababisha malalamishi kutoka kwa wakulima na wanasiasa kutoka maeneo kunakokuzwa chai kwa wingi huku baadhi ya wakulima wakisemekana kuanza kung’oa mimea ya majanichai.

Uchunguzi

Kwa upande wake Bw Maina alimtaka Mkurugenzi wa DCI George Kinoti kuanzisha uchunguzi wa kile alichokitaja kama ufisadi katika usimamizi wa KTDA.

“Huku Rais akiendelea na mchakato wa kuunda jopokazi la kuchunguza yale yanaisibu sekata ya majani chai kwa ujumla, tunamtaka DCI kuanza kuwaandama matapeli ambao wamekuwa wakiwatapeli wakulima katika KTDA. Inakuwaji kwamba mwaka huu KTDA ilichukua asilimia 45 ya Sh80 bilioni ilizopokea kutokana na mauzo ya chai huku ikitoa malipo duni kwa wakulima wetu?” akauliza Bw Maina.

Senata huyo wa Nyeri pia aliitaka mamlaka hiyo kusitisha uchaguzi wa maafisa wake katika ukanda wa Mlima Kenya hadi baada ya maafisa wa sasa kuchunguzwa.

“Kampeni za uchaguzi huo zimeshamiri ufisadi hivi kwamba wajumbe wanapewa hongo ya kima cha Sh1 milioni kila mmoja. Hii inaonyesha wazi kwamba watu fulani wanataka kushikilia nyadhifa katika KTDA ili waendelea kuwapunja wakulima” akasema Bw Maina.

Hata hivyo, wanachama wa bodi ya KTDA Francis Macharia na Erustus Gakuya wameitetea asasi hiyo wakisema kushuka kwa malipo ya bonasi kwa wakulima kulichangiwa kushuka kwa bei ya majanichai katika masoko ya kigeni. Hii ni kutokana na misukosuko ya kisiasa inayoshuhudiwa kwa mataifa yanayonunua chai ya Kenya kwa wingi kama vile Misri, Pakistan, Muungano wa Milki za Kiarabu (UAE) na Sudan Kusini.