Habari

Maseneta wamuunga Yatani kuzinyima fedha kaunti zenye malimbikizo ya madeni

November 26th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MPANGO wa Wizara ya Fedha wa kuzinyima fedha serikali 15 za kaunti ambazo hazijalipa madeni yao umepata uungwaji mkono Jumanne kutoka kwa maseneta.

Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti wamesema hatua hiyo itakuwa funzo kwa kaunti ambazo zimekuwa zikiwadhulumu wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuchelewesha malipo yao.

“Sisi seneti tunaunga mkono mpango huu wa Wizara ya Fedha kwa sababu itakuwa afueni kwa wafanyabiashara wadogowadogo kule mashinani; wengi wao wakiwa vijana na akina mama,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo seneta Mohamed Maalim Mahamud (Mandera).

Amesema hayo katika majengo ya bunge wakati Kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yatani amewasilisha rasmi stakabadhi yenye ombi la kutaka wizara ichukua hatua dhidi ya kaunti zilizokataa kulipa madeni tangu 2013.

Waziri Ukur Yatani (kati). Picha/ Charles Wasonga

Kaunti hizo ni pamoja na Narok, Machakos, Nairobi, Vihiga, Isiolo, Tana River, Migori, Tharaka-Nithi, Bomet, Kirinyaga, Nandi, Mombasa, Kiambu, Garissa, na Baringo.

Na huku akiunga mkono mpango huo, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula amemtaka kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yatani kuhakikisha adhabu hiyo haiathiri fedha zinazolenga kufadhili utoaji wa hudumu muhimu kama afya.

“Bw Waziri, hatua hii ni nzuri, lakini unapasimamisha utoaji wa fedha kwa kaunti ambazo hazijalipa wakandarasi na wafanyabiashara wadogowadogo tunaomba fedha za sekta muhimu kama afya na mishahara ya wafanyakazi zisiguzwe,” akasema.

Kulingana na Bw Yatani, kufikia mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020 wakandarasi na wafanyabiashara mbalimbali walikuwa wakizidai kaunti hizo jumla ya Sh51 bilioni.