Habari MsetoSiasa

Maseneta wanavyotumia utata wa ugavi wa mapato kujijenga

August 9th, 2020 3 min read

Na WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA kuwa baadhi ya maseneta wanatumia utata uliopo kuhusu Mfumo wa Ugavi wa Mapato kwa serikali za kaunti kujijenga kisiasa ielekeapo 2022.

Maseneta wamelazimika kuahirisha vikao kujadili kuhusu mfumo huo kwa mara saba, ambapo sasa Seneti imeamua kubuni kamati maalum itakayojaribu kutatua mzozo huo.

Hata hivyo, imefichuka kwamba wengine wao wamekuwa wakifanya hivyo kimakusudi ili kuimarisha mwonekano wao kisiasa, kwani wanalenga kuwania nyadhifa mbalimbali za kisasa, hasa ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Miongoni mwa maseneta ambao wameibukia kuwa wenye usemi mkubwa kuhusu mfumo huo ni Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Cleophas Malala (Kakamega), Johnson Sakaja (Nairobi), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Kindiki Kithure (Tharaka Nithi), Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata kati ya wengine.

Hata hivyo, maswali yaliyopo ni kuhusu sababu za baadhi yao kujitokeza pakubwa kuupinga mfumo huo, licha ya kaunti zao kuwa miongoni mwa zile zinazofaidika kwa kuongezewa mgao wa fedha zitakazotolewa na Serikali Kuu.

Sababu nyingine ni baadhi yao kujitokeza wazi kukaidi misimamo ya vyama vyao kama Jubilee na ODM, licha yavyo kutangaza hadharani kuhusu kuunga mkono mfumo huo.

Wengine wameapa kiwazi kuwakaidi Rais Uhuru Kenyatta, Mabwana Raila Odinga na Kalonzo Musyoka, ambao ni viongozi wa vyama vya Jubilee, ODM na Wiper mtawalia.

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema maseneta hao wanaiga mbinu za watangulizi wao kwenye muhula uliopita (2013-2017), kujisawiri kama “wazalendo” na “watetezi” wa wananchi, huku wengi wakilenga kuwania ugavana katika kaunti wanazotoka.

Baadhi ya maseneta wa awali waliofaulu kutwaa nafasi za ugavana kwenye uchaguzi wa 2017 ni Mike Sonko (Nairobi), Kiraitu Murungi (Meru) na Stephen Sang (Nandi).Wengine walishindwa walipojaribu kuwania.

Baadhi yao ni Muriuki Karue (Nyandarua), Lenny Kivuti (Embu), Hassan Omar (Mombasa), Waziri wa Afya Mutahi Kagwe (Nyeri) kati ya wengine.

Kwa mujibu wa wadadisi, maseneta waliofanikiwa kuchaguliwa kama magavana walitumia nafasi zao kwenye Seneti ‘kuwaingilia kisiasa’ magavana waliokuwa vitini, ikizingatiwa moja ya majukumu makuu ya Seneti ni kuangalia utendakazi wa serikali za kaunti.

“Magavana kama Sonko na Sang walichaguliwa kwa kujisawiri kama watetezi wa wananchi na ‘wafichuzi’ sakata za ufisadi dhidi ya magavana Evans Kidero na Cleophas Lang’at. Hilo liliwapa umaarufu sana miongoni mwa wananchi, kwani walichora taswira ya kuwa wanaojali maslahi ya wenyeji,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanaeleza kuwa sawa na watangulizi wao, lengo kuu la maseneta wanaopinga mfumo huo ni kuhakikisha wametumia nafasi kupanua mwonekano wao.

Wanaeleza kuwa katika muhula uliopita, baadhi ya maseneta ndio walikuwa chanzo kikuu cha masaibu yaliyowakumba magavana, ambapo wengi walitakikana kufika mbele ya Seneti ‘kujibu maswali kuhusu walivyotumia fedha za kaunti.’

“Maseneta wengi walijificha nyuma ya masaibu yaliyowakumba magavana hao kama njia ya kuendeleza kampeni zao kichinichini. Hili ndilo liliwafanya magavana kama Kidero (Nairobi), Dkt Langat (Nandi), Peter Munya (Meru) kati ya wengine kutochaguliwa tena,” asema Bw Muga.

Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa, anasema kuwa kwa kupinga mfumo huo, wanafanya hivyo pia kutokana na mazingira yaliyopo kuhusu janga la corona.

“Wengi wamebaini kwamba hii ndiyo nafasi pekee waliyo nayo kuanza kampeni zao kwani imebaki miaka miwili tu kabla ya uchaguzi wa 2022. Vile vile wanafanya hivyo kwani wanasiasa hawawezi kufanya mikutano ya kisiasa kutokana na janga la virusi vya corona,” asema Bw Bigambo.

Tayari, baadhi ya maseneta wameonyesha azma za kuwania ugavana katika kaunti zao, ingawa hawajatangaza waziwazi.Kwa mfano, katika Kaunti ya Nairobi, Bw Sonko amekuwa akimlaumu Seneta Sakaja kuwa moja ya ‘chanzo’ cha masaibu yanayomkumba, akimlaumu kwa kuendesha juhudi za kichinichini kupanga mikakati ya kushindana naye 2022.

Katika Kaunti ya Nandi, Seneta Samson Cherargei amekuwa moja ya wakosoaji wakubwa wa Gavana Sang’, kiasi kwamba ilibidi Naibu Rais William Ruto kuingilia kati ili kutatua uhasama baina yao.

Seneta Cherargei pia ameibukia kuwa miongoni mwa maseneta wanaounga mkono mfumo huo na mtetezi mkubwa wa Dkt Ruto.Katika Kaunti ya Nakuru, Gavana Lee Kinyanjui amekuwa akimlaumu Seneta Susan Kihika kwa kutumia Seneti kama jukwaa la kuendesha ‘kampeni za ugavana’ kwa kuisawiri serikali yake kuwa isiyowajali raia.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi na wataalamu wa masuala ya utawala wanaitaja hali isyofaa kwa mfumo wa ugatuzi, kwani wananchi ndio watakaoumia kwa kukosa huduma bora.

“Ingawa nyadhifa hizi zote ni za kisiasa, si taswira nzuri wakati magavana na maseneta wanaanza kuvutana kisiasa zaidi ya miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Kunapaswa kuwa na masharti makali yatakayohakikisha kuwa viongozi hawatumii nafasi zao kuwaingilia wengine ili kufanikisha lengo kuu la mfumo wa ugatuzi,” asema Bw Felix Onyango, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya utawala.