Habari

Maseneta wapinga sera ya serikali ya kuajiri wafanyakazi kwa kandarasi ya miaka mitatu

June 21st, 2019 1 min read

MASENETA wamepinga tangazo la serikali kwamba itaanzisha mpango wa uajiri wa watumishi wa umma kwa kandarasi kuanzia Julai 1, 2019, kama hatua ya kuleta mageuzi katika sekta ya utumishi wa umma.

Walisema shughuli hiyo haifai kuharakishwa kwani huenda ikaleta madhara kwa wafanyakazi husika na hatimaye kuathiri uchumi wa nchi.

“Suala la mzigo wa ulipaji mishahara linafaa kushughulikiwa kwa makini na wala sio kupitia maamuzi ya ghafla ambayo hayawezi kuisadia taifa kutatua suala hili,” akasema Seneta Johnston Sakaja ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Leba.

“Tangazo hilo pia lilitolewa kabla ya serikali kuhakikisha kuwa mpango huo unahimiliwa kwenye sheria. Ikiwa shughuli hiyo itatekelezwa ilivyotangazwa, basi serikali itakuwa imekiuka sheria za Leba na Katiba,” akasema Bw Sakaja aliyeongea na wanahabari Alhamisi kwa niaba ya wanachama wa kamati yake.

Unyanyasaji

Kamati hiyo pia ilionya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) dhidi ya kutumia mpango huo kama hatua ya kuwaadhibu au kuwanyanyasa wafanyakazi wa umma.

PSC ilisema kuwa kuanzia Julai mosi mwaka huu, watumishi wa umma watakuwa wakiajiriwa kwa kandarasi ya miaka mitatu. Pia kandarasi hizo zinaweza tu kuongewa kwa miaka mingine mitatu ikiwa wafanyakazi husika watatimiza malengo ya utendakazi waliyowekewa.

Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) pamoja na vyama vingine vimepinga mpango huo vikidai haufai.