Habari Mseto

Maseneta wataka kafyu zilizowekwa ziondolewe

January 14th, 2024 2 min read

NA COLLINS OMULO

MASENETA wanaitaka serikali ya kitaifa kufanyia marekebisho sheria za kafyu wakisema nyingi zimekosa kutimiza wajibu wake.

Wameitaka serikali kutathmini na kuwekeza katika mikakati ya wanajamii na hatua nyingine badala ya kutegemea kafyu pekee.

Walisema kuna sababu za kutosha za Wizara ya Usalama wa Ndani kutafakari kusitisha kafyu kwa sababu baadhi zimeweza tu kuzuia shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyoathirika.

Haya yamejiri wakati Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki akitangaza kafyu katika maeneo ya Mashariki yanayojumuisha Isiolo, Samburu na Marsabit ambako mamia ya watu na maelfu ya ng’ombe waliuawa katika siku za hivi majuzi.

Hii ni pamoja na kafyu zinazoendelea ambazo zimewekwa eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambalo limegubikwa na ujangili na wizi wa mifugo.

Seneta wa Kaunti ya Turkana James Lomene alisema pana haja ya dharura kukomesha kafyu hizo katika miji na vituo vikuu katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, hususan Kaskazini mwa Bonde la Ufa hasa Kaunti ya Turkana.

Inaonekana agizo hilo limeshindwa kutekeleza majukumu yake na huenda hata linasababisha madhara zaidi kwa kuathiri maisha ya familia, usalama na uzima wa wakazi.

Alihoji kuwa lengo kuu la kafyu katika maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama ni kuimarisha usalama na kulinda raia dhidi ya hatari inayoweza kuzuka.

Hata hivyo, amedai kuwa kafyu hiyo haitimizi malengo yake hivyo basi hatua ya kuiendeleza huenda ikazua maswali.

Ingawa hivyo, amesema visa vya uhalifu katika saa za kafyu vimeongezeka katika mitaa kama vile Lokichar, Kalemngorok na Kainuk ikilinganishwa na saa zisizo za kafyu.

“Pana sababu kadhaa za kuzingatia kukatiza kafyu katika maeneo yanayokumbwa na ukosefu wa usalama eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kwa sababu inaonekana kushindwa kutekeleza malengo yake na badala yake kusababisha madhara zaidi kushinda mema,” alisema Bw Lomenen.

Kukiwa na dhana kuwa kafyu hazichangii chochote kuimarisha usalama, hatua ya kuiondoa huenda ikawa mwafaka ili kuzuia taharuki kupanda.

Seneta wa Tana River Danson Mungatana alirejelea kauli ya mwenzake akisema kafyu zimeathiri biashara.

Akitaja kisa cha Lamu, alisema Waziri anapotoa maagizo kama ya kupiga marufuku uvuvi au usafirishaji wa wanyama, amri hiyo huathiri kiasi biashara eneo hilo.