Habari za Kitaifa

Maseneta wataka makuhani wa mbolea feki wakamatwe

April 1st, 2024 2 min read

NA COLLINS OMULO

MASENETA sasa wanataka maafisa wa serikali walioruhusu mbolea duni kuingia nchini na katika mabohari ya Bodi la Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) washtakiwe.

Wawakilishi hao vilevile wanataka maafisa husika, wakipatikana na hatia, wawarejeshee pesa wakulima walionunua mbolea hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, James Murango, amesema wameanzisha uchunguzi kuhusu jinsi mbolea hiyo feki ilivyoingia nchini huku wakimulika Shirika linalosimamia Viwango vya Ubora Nchini (Kebs) na Shirika la Kitaifa kuhusu Biashara Nchini (KNTC).

Seneta huyo wa Kaunti ya Kirinyaga amesema wizara za kilimo na biashara zinaangaziwa kuhusiana na sakata inayoendelea kwa sababu mbolea hununuliwa kupitia KNTC huku Kebs ikihitajika kukagua ubora.

Aidha, alisema wakulima kote nchini wameripoti kununua mbolea kutoka mabohari ya NCPB na wala sio maduka ya kuuzia pembejeo za kilimo.

“Kilio cha mbolea feki kimetufikia. Kama Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo, tunataka kuchunguza ili tujue ikiwa kuna hujuma. Iwapo ni hujuma, basi mbolea hiyo ilifikaje katika mabohari ya NCPB? Tunataka kujua ni vipi Kebs haikuwa na habari kwamba mbolea ghushi ilikuwa inasambaziwa wakulima,” alisema Bw Murango.

Seneta huyo alihoji kwamba, hata ikiwa mbolea hiyo ghushi ilipakiwa nchini, swali kuu ni jinsi mbolea hiyo iliweza kupenya katika mabohari ya NCPB yanayomilikiwa na serikali bila kugunduliwa.

“Wasambazaji hao wa bidhaa wanaoleta mbolea hutangaza nembo zao, kuna ukaguzi na vipimo vya kuhakikisha ubora, kwa hivyo iliwezaji kukwepa Kebs na mashirika mengine kiasi cha kufikia wakulima?” alihoji.

Seneta huyo amesema hawawezi kupuuza uwezekano kuwa baadhi ya maafisa fisadi serikalini wanahusika na sakata hiyo ili kupata hela akisema watakaopatikana na hatia wanafaa kufidia wakulima ikiwemo kuwapotezea fursa ya kulima na kuuza mazao yao.

“Walionunua mbolea hiyo walifanya hivyo kupitia NCPB. Tunataka kujua ni vipi na ni lini wanaweza kurejeshewa hela zao au kupatiwa mbolea inayofaa. Wana risiti za kununua na mbolea inayoweza kupelekwa kwenye maabara kufanyiwa vipimo,” alisema Seneta huyo.

“Unaweza tu kutetea jambo baada ya kujua kilichofanyika. Wakulima hawa wote sio wendawazimu kusema waliuziwa mbolea ghushi,” alisema.

Alisema Kamati imemwalika Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, kufika mbele yake wiki hii ili kufafanua kuhusu suala hilo la mbolea ghushi baada ya kukosa kujitokeza Alhamisi iliyopita (Machi 28, 2024).

“Wakulima wengi wanagundua tatizo hilo baada ya kununua mbolea. Wanafungua mifuko na kupata mchanga, kinyesi cha punda na mawe. Inahuzunisha sana,” alisema Bw Murango.

“Serikali kupitia wizara husika inapaswa kuwajibika. Wakulima hawafai kuteseka kwa sababu ya utepetevu wa baadhi ya maafisa wa serikali.”

Seneta wa Kaunti ya Makueni, Dan Maanzo, alisema maafisa husika wanapaswa kutiwa mbaroni na Idara ya Mashtaka kuhusu Uhalifu (DCI) ipendekezewe washtakiwe.