Habari Mseto

Maseneta waunda kikao kingine cha upatanisho

August 18th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine maseneta wamebuni kamati ya upatanishi kujaribu kusaka mwafaka kuhusu suala tata la mfumo wa ugavi wa fedha katika kaunti.

Hii ni baada ya wao kukosa kuelewana kwa mara ya tisa kuhusu suala hilo katika kikao maalum cha Jumatatu, Agosti 17, 2020.

Hoja ya kubuniwa kwa kamati hiyo ya maridhiano iliwasilishwa na kiongozi wa wengi James Orengo Jumatatu jioni baada ya maseneta hao kuahirisha kikao kwa dakika 30 kufanya mkutano wa faragha kusaka mwelekeo.

Kulingana na Bw Orengo waliafikiana kuwa wanachama wa kamati hiyo watakuwa maseneta wafuatao; Johnston Sakaja (Nairobi). Mohammed Mahmud (Mandera), Stewart Madzayo (Kilifi), Kipuchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Susan Kihika (Nakuru).

Wengine ni pamoja na; Moses Kajwang (Homa Bay), Anuar Oloitiptip, Moses Wetang’ula (Bungoma), John Kinyua (Laikipia) na Ledama Ole Kina (Narok).

Bw Orengo ambaye ni Seneta wa Siaya alitangaza kuwa washirikishi wenza wa kamati hiyo watakuwa Mbw Wetang’ula na Sakaja.

Na wasaidizi wa kamati hii wataongozwa na Karani wa Seneti Bw Jeremiah Nyengenye.

“Na tumekubaliana kwamba kamati hii itafanya kikao cha kwanza Jumanne saa nane na nusu ili kupanga ratiba ya shughuli zake. Baadaye watatueleza ni lini tutafanya Kamukunji kabla ya kufanya kikao kingine maalum mnamo Jumanne wiki ijayo,” akasema Bw Orengo.

“Niko na matumaini kuwa kwa utaratibu huu tutaweza kuelewana wiki ujao tukikutana,” akaongeza.

Hoja hiyo iliungwa mkono na maseneta wa mirengo yote miwili katika suala hilo wakiongozwa na kiongozi wa wengi Samuel Poghisio.

Hata hivyo, Bw Poghisio alionya kuwa kikao maalum hakipasi kufanyika Jumanne wiki ijayo kabla ya wao kupata mwafaka kuhus suala hilo.