Michezo

Mashabiki 200,000 watia saini Sergio Ramos aadhibiwe kwa kumuumiza Salah

May 28th, 2018 2 min read

Na MASHIRIKA

DIFENDA wa Real Madrid Sergio Ramos amejipata matatani baada ya mashabiki kote ulimwenguni kuanzisha kampeni ya kutaka aadhibiwe kwa kumjeruhi straika wa Liverpool Mohamed Salah kwenye fainali ya Klabu Bingwa Uropa jijini Kiev, Ukraine.

Si mara ya kwanza kwa difenda huyo kuumiza mchezaji, hulka ambayo inafanya mashabiki nje ya Madrid kumshobokea kutoka na mbinu zake za uchezaji zinazolenga kuumiza na kuwapa kadi wapinzani.

Tangu tukio hilo la Jumamosi usiku, Ramos amekuwa adui mkubwa wa ulimwengu wa soka, licha ya Real Madrid kuikomoa Liverpool 3-1.

Mshambulizi huyo ya Misri aliangushwa na Ramos huku akimvuta mkono na kumlalia hali iliyopelekea jeraha na uchungu mwingi uliomlazimisha kuondoka uwanjani.

Sasa mashabiki wameungana mtandaoni kupitia kwa tovuti ya change.org ambapo wametia zaiidi ya saini 200,000 wakiitaka shirika linalosimamia shindano hilo, UEFA na FIFA kumchukulia hatua kali za kinidhamu difenda huyo.

Mwasisi wa kampeni hiyo, Mohamed Salah Abdel-Hakeem, alisema: “Ramos alimuumiza Salah kimakusudi na kushindia kujifanya kuwa aliangushwa na wachezaji wa Liverpool, na kufanya Sadio Mane alishwe kadi ambayo hakustahili.”

“Sergio Ramos alionyesha mfano wa kinyama kwa wachezaji wa usoni wa soka. Badala ya kushinda mechi kihalali, yeye hutumia mbinu za hila ili kuvunja nguvu za timu pinzani.

“UEFA na FIFA zinafaa kumchukulia hatua kali sana Ramos na wachezaji wenye tabia sawa, wakitumia video za tukio hilo, ili kurejesha nidhamu ya soka.”

Hakuna yeyote mwenye hai ya kusema kuwa Ramos alisababisha jeraha hilo kimakusudi, hata kama ana historia ya kuwajeruhi wapinzani, lakini mashabiki sasa wanataka atiwe adabu.

Kwingineko, nahodha wa timu ya Italia Leonardo Bonucci amesema kuwa anaamini straika mtatanishi Mario Balotelli amekomaa, huku akijiandaa kuiwakilisha Italia kwa mara ya kwanza kwa miaka minne.

Kocha mpya wa Azzurri, Roberto Mancini alisimamia mechi ya kwanza ambayo timu hiyo iliyoshinda Kombe la Dunia mara nne, ilipiga dhidi ya Saudi Arabia jana usiku jijini Saint Gallen, Switzerland. Hata hivyo, Italia haikufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka huu.

Mancini alimuita straika huyo wa Nice kikosini kwa mechi tatu za kirafiki zijazo baada ya kuachwa nje na Italia kutokana na majeraha na mienendo ya ukosefu wa nidhamu uwanjani.

“Nimepata kwamba Mario amebadilika sana ikilinganishwa na awali, amekomaa,” akasema Bonucci kabla ya mechi.

Super Mario ametikisa nyavu mara 13 katika mechi 33 ambazo ameichezea timu ya taifa lakini hajaitwa kikosini tangu Italia iondolewe kutoka kwa Kombe la Dunia 2014 katika mechi za makundi.

“Yeye ni mmoja wa mastraika wazuri zaidi na tunatarajia kuwa atatuletea matokeo bora kwa mechi za usoni kwa bado ni machachari,” akasema Mancini.
Katika

“Hii nimechi ya kwanza kwa hivyo ni lazima tuanze vizuri, na haimaanishi kushinda pekee. Cha muhimu ni vijana kucheza bila presha na kuepuka kufanya masihara,” akaongeza.

Italia itacheza mechi ya tatu ya kirafiki Juni 4 dhidi ya Uholanzi ambayo pia haikufuzu kwa kipute cha Urusi.