Bambika

Mashabiki hawapati picha kabisa Bensoul kutema Noni Gathoni na kuchukua beste yake Cindy K

April 17th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO

WASWAHILI wanasema kikulacho ki nguoni mwako. Ni methali ambayo staa wa zamani wa Sol Generation Bensoul anaifahamu vyema ila ameamua kuipuzilia mbali.

Hii ni baada yake kuingia kwenye penzi nzito na msupa mtengenezaji maudhui maarufu Cindy Kipsang almaarufu Cindy K.

Utata upo kwamba huyu Cindy K, aliwahi kuwa swahiba wake Noni Gathoni ambaye kwa muda mrefu alikuwa ni demu wake Bensoul.

Kuna kipindi mahusiano ya Bensoul na Gathoni yalikuwa yameshamiri kiasi cha yeye kuahidi kumwoa. Lakini hilo halikutokea penzi lao likiishia kuingia mdudu na kuwapelekea kuachana.

Hii ndio sababu wengi hawapati picha kabisa baada ya Bensoul kuweka wazi kuwa yeye na Cindy K kwa sasa wana mahusiano ya kimapenzi.

Lakini Bensoul anasema, hajali wala hataki kusikia chochote kutoka kwa yeyote anayekusudia kukashifu penzi lake jipya.

“Yule ni demu wangu na ni mtu wa mwema. Tumekuwa tukitoka kwa muda sasa na haijalishi ambacho mtu yeyote atataka kusema kutuhusu. Kama unataka kukashifu, una ruksa we kashifu tu, haitatuumiza, haitatupunguzia penzi,” Bensoul kamwaga yake ya moyoni.

Mkanganyiko hata zaidi ni kwamba Bensoul bado ni swahiba mkubwa wa YouTuber, Prince Newton. Newton ni ex wake Cindy K.

Cindy K ambaye sio mgeni kwenye drama hizi za mapenzi, alianza kutoka na Newton baada ya kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Shaq The Yungin.

Shaq na Newton waliwahi kuwa marafiki wa kufa kuzikana, uswahiba uliovunjika baada ya Shaq kudai kuwa Cindy K alikuwa akimchepukia na rafiki yake huyo.

Bensoul na Cindy K waliamua kuitangazia dunia kwamba wanadeti kwenye tamasha la Raha Fest lililofanyika wiki iliyopita ambapo mwimbaji huyo alimpandisha jukwani Cindy K na kisha kumbeza kwa kumwimbia wimbo wa mapenzi kabla ya kutuza na rundo la maua.