Michezo

Mashabiki wa Gor Mahia wasema kuondoa USM Alger ni muujiza

September 17th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KICHAPO cha Gor Mahia cha mabao 4-1 mikononi mwa wenyeji wao USM Alger ya Algeria katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika (CAF), duru ya kwanza ya raundi ya kwanza mnamo Jumapili usiku, kimegawanya mashabiki wake.

Baadhi ya mashabiki hao wanaofahamika kwa jina la utani kama Green Army, wanaamini bado Gor ina matumaini ya kulipiza kisasi katika mechi ya marudiano jijini Nairobi hapo Septemba 29. Ikishinda Waalgeria hao kwa mabao 3-0, itaingia katika mechi za makundi za Klabu Bingwa.

Vijana hao wa kocha Steven Pollack wasipopata ushindi huo mkubwa jijini Nairobi, basi watateremka katika mashindano ya daraja ya pili, ambayo ni Kombe la Mashirikisho.

Hapa pia watahitajika kupiga mshindi kwa mechi za raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho ili kuingia mechi za makundi.

“Matumaini bado yapo. Tujazeni uwanja wa Kasarani wakati wa mechi ya marudiano na kuwapa vijana wetu motisha,” alisema DO Aboka kabla ya kuongeza, “Natumai kocha na msaidizi wake watarekebisha makosa mengi tuliyofanya katika safu ya ulinzi pamoja na idara ya kulinda lango.”

Judith Nyangi anaamini Gor itatesa vilivyo nyumbani. Alikuwa na maneno machache kuhusu mechi ya marudiano akisema “Kasarani itakuwa kisirani.”

Hata hivyo, sauti kubwa ya mashabiki inatoka kwa wanaoamini Gor imeshaaga Klabu Bingwa.

Kevin Reyes Odu alisema, “Gor imebanduliwa nje. Huo ndio ukweli mchungu.”

Stalin Matididi Mbappe, “Tusidanganye… Gor imeshatolewa katika Klabu Bingwa kabla hata ya mechi ya marudiano. USM Alger inakuja kukamilisha kazi jijini Nairobi.” Wengi wa mashabiki, ambao wanaamini Gor haiendi mahali katika Klabu Bingwa msimu huu, wameitaka ianze kuweka akilini mwake jinsi inavyoweza kushindania taji la Kombe la Mashirikisho.

Aidha, mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa Kenya wa msimu 2018-2019 ya wanahabari wa michezo (SJAK) Joash Onyango pamoja na kipa mpya David Mapigano wamekosolewa vikali na mashabiki kwa kazi yao.

Shabiki Moses Oyolla aliashiria Onyango ameshuka kimchezo akisema, “Joash Onyango almaarufu Berlin Wall tuliyemjua msimu uliopita si ambaye tuko naye wakati huu! Kocha anafaa kumtumia (Shafik) Batambuze kama amepona jeraha.”

Makosa kadha ya Mapigano yaliyochangia Gor kufungwa yalimfanya kushambuliwa kwa maneno na Jackson Ouma. Alimtaja kama “feki” na kutaka Peter Fredrick Odhiambo arejeshwe michumani. Mapigano alitua Gor wiki chache zilizopita kutoka Singida United nchini Tanzania.

Rachier alaumiwa

Ofisi ya Gor inayoongozwa na Ambrose Rachier pia haikuepuka lawama.

“Wachezaji 11 wa kwanza hawana uzoefu na ujuzi unaohitajika kudhibiti presha katika kiwango cha Klabu Bingwa. (Kenneth) Muguna na Joash (Onyango) pekee ndio wana sifa hizi. Ilikuwa kosa kuagana na wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza na kutarajia muujiza,” alichemka Sen Ajowi K’ochollah.

Collins Koyo alikuwa na maoni sawa na hayo. Alisisitiza kuwa kufanyia kikosi mabadiliko makubwa kila msimu kunachangia Gor kuwa na wachezaji wasio na ujuzi wa kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kabla ya msimu 2018-2019 kuanza, Gor ilipoteza mfumaji hodari Meddie Kagere na mambo hayakuwa tofauti ikianza msimu huu bila nyota mwingine kutoka Rwanda, Jacques Tuyisenge pamoja na wachezaji tegemeo kama Harun Shakava na Francis Kahata walioamua kuvuka mpaka kusakata soka yao ya malipo nchini Angola, Zambia na Tanzania, mtawalia.

Dhidi ya USM Alger, Muguna alifungia Gor bao la ugenini kupitia penalti dakika ya 56. Mohamed Meftah na Zakaria Benchaa walifungia USM Alger mabao mawili kila mmoja.