Michezo

Mashabiki wa Leicester City walaumiwa

December 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MASHABIKI wa Leicester City wameshutumiwa vikali kwa kuzoea kuondoka uwanjani mapema kabla ya mechi kumalizika.

Kocha Brendan Rodgers alitoa shutuma hiyo jana baada ya mashabiki hao kuondoka uwanjani dakika chache kabla ya Kelechi Iheanacho kufunga bao ushindi dakika ya 85 katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Everton, Jumapili.

“Ujumbe wangu ni: ‘Mashabiki, acheni kuondoka uwanjani mapema,'” Rodgers alisema.

“Hii ni timu ambayo hata ikiwa inaongoza kwa 9-0 au 1-1, tunawahitaji hadi dakika ya mwisho. Timu inacheza kwa bidii. Nafurahia kuona mashabiki wakishangilia na ningependa kuwaona wakibakia uwanjani hadi dakika ya mwisho. Lazima waelewe tuko na timu inayopigana vikali hadi dakika ya mwisho. Wasiwe wanakata tamaa hata tunapokuwa 1-1 dakika ya mwisho wasiwe.”

Wakati huo huo, kocha Jose Mourinho wa Tottenham Hotspur amesema kwamba hakuna kocha atakayekaa usukani kwa miaka mingi kwenye ligi kuu ya Uingereza (EPL) kama walivyokaa wakongwe Arsene Wenger na Alex Ferguson.

Mourinho ambaye majuzi alipewa jukumu la kuokoa Spurs baada ya Mauricio Pochettino kufutwa alisema Wenger atakuwa kocha wa mwisho katika zama hizi huku akiongeza kwamba haoni kama kutatokea mwingine atakayedumua kama Mfaransa huyo pamoja na Alex Ferguson aliyekuwa na Manchester kwa kipindi cha miaka 26.

Mourinho alisema Wenger ndiye kocha aliyefanikiwa zaidi katika historia ya Arsenal ambapo alishinda mataji 17 katika kipindi cha miaka 22 kabla ya kuondoka msimu wa 2017/2019.

Kinyume na Wenger, Mourinho amefundisha timu tisa tofauti katika kipindi cha miaka 19 kabla ya kupewa jukumu la kocha Pochettino kuifundisha Spurs.

Alipoulizwa kama kutakuja kutokea makocha kama Wenger na Ferguson, Mourinho alisema: “Miaka 20 katika klabu kimoja sio rahisi siku hizi. Hivyo sidhani kama ni rahisi kutokea tena.”

Hata mitazamo ya watu ni tofauti. Kuna mahusiano ya haraka, watu wanachoka kirahisi hata mazoezini pengine kutokana na vyakula vya siku hizi. Hivyo, nadhani Wenger ni wa mwisho.

Mourinho anaamini kiwango cha kutathmini makocha kwenye soka la kisasa ina maana makocha wa EPL wako kwenye shinikizo kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa zamani nyakati za akina Wenger.