Michezo

Mashabiki wa Manchester United ndio watundu zaidi – Ripoti

June 19th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MASHABIKI wengi wa Manchester United ndio ambao wamekuwa wakikamatwa kuhusiana na visa vya ubaguzi wa rangi, zaidi kuliko wa timu nyinginezo nchini hapa, katika misimu minne, hii ni kulingana na utafiti wa Home Office.

Ripoti ya Freedon of Information kwa ombi la Presss Association imeonyesha kwamba mashabiki 27 waliopatikana kuwa wafuasi wa klabu ya Manchester United walikamatwa na polisi wakati wa misimu ya 2014-15 hadi 2017-18.

Klabu hiyo inafuatiwa na Leeds United na Millwall za Daraja la Kwanza baada ya mashabiki wao 15 mtawalia kukamatwa wakati wa kipindi hicho, huku Leicester City ikifuata na 14 halafu Chelsea 13.

Visa vibaya zaidi vya ubaguzi wa rangi vilitokea msimu huu wa 2018-19, lakini habari zake kamili zitatolewa rasmi baadaye.

Wakati ripoti hiyo ikitolewa, Manchester United kupitia kwa msemaji wao imedai klabu yao inaongoza kwa visa hivyo kwa sababu ya idadi yao kubwa ya mashabiki ambao wamesambaa kila mahali duniani.

“Hatukubalii tabia hii, na tuko tayari kabisa kupiga vita mambo kama haya kwa lengo la kuufanya mchezo wa soka kuvutia bila ubaguzi kupitia kwa mwito wetu wa All Red All Equal wa kupinga ubaguzi wa rangi michezoni.

Inaeleweka kuna mashabiki wa nyumbani wapatao 69,000 miongoni mwa 72,000 kila wakati mechi inapochezewa Old Trafford, na zaidi 3,000 katika mechi yoyote ya ugenini.

‘Muda wa kuondoka umefika’

Wakati huo huo, kiungo wa Manchester United, Paul Pogba amesema muda wake wa kuondoka Old Trafford umefika.

Tayari Mfaransa huyo amehuzunishwa na klabu ya Real Madrid ya Uhispania pamoja na Juventus ya Italia.

Nyota huyo ambaye ndiye pekee kutoka klabu ya Manchester United aliyejumuishwa kwenye kikosi bora cha ligi msimu huu wa 2018-19 angali na mkataba wa kuichezea Manchester United hadi 2021.

“Naomba waniachilie nijaribu maisha sehemu nyingine,” staa huyo mwenye umri wa miaka 26 aliwaambia waandishi.

“Nimekuwa hapa kwa miaka mitatu, na maisha yamekuwa mazuri, lakini nataka kuondoka sasa kama ilivyo kwa watu wengine pia. Nikiondoka, nafikiria kwangu litakuwa jambo jema kupata tajriba mpya.”

Lakini wakuu wa Manchester wanataka staa huyo abakie hadi msimu ujao umalizike baada ya kurejea klabuni mnamo 2016 baada ya kuwa na Juventus kwa misimu miwili.

Majuzi, kocha wa klabu hiyo, Ole Gunnar Solskjaer alisema kuwa kiungo huyo haendi popote kwa sasa.

Pogba aliibukia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Manchester United na kufikia sasa ameichezea klabu hiyo mechi 89 za ligi kuu ya Uingereza na kuifungia mabao 24.