Michezo

Mashabiki wa raga wamwomboleza Richard Sidindi Otieno

February 25th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAPENZI wa raga wanaomboleza kifo cha mchezaji Richard Sidindi Otieno ambaye ameaga dunia Jumatatu asubuhi.

Mwendazake alikuwa mchezaji muhimu wa klabu ya Impala Saracens tangu mwaka 2011 akiichezea katika mechi za Ligi Kuu na mashindano ya Enterprise Cup, raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande pamoja na Bamburi Super Series.

Aliwahi kuitwa katika kikosi cha mazoezi cha timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu msimu 2017-2018 chini ya kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu, ingawa hakupata fursa ya kupeperusha bendera ya Kenya katika Raga ya Dunia.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) limetangaza kifo cha Sidindi likisema kwamba amewacha familia changa ya mke mmoja kwa jina Catherine na mtoto Candace. “Mipango ya mazishi itatolewa baadaye,” KRU imesema kupitia taarifa kutoka klabu ya Impala Saracens.

Tovuti ya ragahouse.com inasema kwamba mchezaji huyu wa zamani wa Shule za Upili ya Upili ya St Mary’s Yala na Chuo Kikuu cha Maseno amefariki akifanya mazoezi ya kuogelea. Huenda alikufa maji. Hakushiriki mechi kati ya Impala na Homeboyz mnamo Februari 23 ambayo klabu yake ilishinda 36-27 uwanjani Impala Grounds jijini Nairobi. Mechi yake ya mwisho ilikuwa Februari 16 dhidi ya mabingwa watetezi KCB ambayo klabu yake ilipoteza 25-3.