Michezo

Mashabiki wachemkia Kimanzi baada ya Stars kupoteza mechi

October 15th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

JE, ilikuwa kosa kumuajiri tena Francis Kimanzi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya almaarufu Harambee Stars?

Mashabiki wanaonekana kuamini hivyo. Wengi waliozungumza baada ya Stars kupoteza 1-0 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Msumbiji hapo Jumapili, wameelekeza lawama zao kwa kocha huyu wa zamani wa klabu za Sofapaka, Tusker na Mathare United.

Kimanzi, 43, aliwahi kuongoza Stars mwaka 2008-2009 na tena 2011-2012 kabla ya kutwikwa majukumu ya kocha mkuu tena mnamo Agosti 20 baada ya Mfaransa Sebastien Migne kutemwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Kandarasi ya Kimanzi ni ya miaka miwili. Hata hivyo, akikaribia kula mshahara wake wa pili, amejipata akiandamwa na shinikizo kwa sababu hana ushindi katika mechi zake mbili za kwanza. Vijana wake walikabwa 1-1 dhidi ya Uganda mnamo Septemba 8 uwanjani Kasarani kabla ya kunyamazishwa mbele ya mashabiki wao uwanjani humu mnamo Oktoba 13.

“Hongera!” shabiki Christian Whitney Oduor aliambia Kimanzi kwenye mtandao wa Facebook wa FKF.

Aliongeza, “Unarejesha Harambee Stars ilikokuwa ulipochagua kikosi bila umakinifu. Sebastien (Migne) alichagua kikosi chake kwa busara, lakini naona umepuuza hili, unaona matokeo yake? Kikosi hiki kitaaibishwa 4-0 na Misri.”

Shake Dennis Dool, “Mambo yalitarajiwa kuwa hivi! Sijui Kimanzi atafikisha wapi soka ya Kenya na matokeo kama haya.”

Ingwe Newton, “Ilikuwa wazi kutoka mwanzo kuwa Kimanzi hatatufikisha popote. Mtu ambaye hakushinda taji muhimu na Mathare. (Rais wa FKF) Nick Mwendwa aliacha kutafuta mtu kama (Jacob) ‘Ghost’ Mulee ambaye anakumbukwa kwa kupata matokeo mazuri na Harambee Stars. Mwendwa anafaa kuelewa kuwa timu hii ni ya taifa na kwa hivyo hawezi kuchagua tu mtu yeyote kuiongoza.”

Baada ya baadhi ya mashabiki kumtetea Kimanzi wakisema apewe muda, Ingwe Newton aliongeza kuwa Kimanzi hafai kutetewa kwa sababu “anafahamu wachezaji wa Kenya vyema. “Kumbukeni pia alihudumu kama kocha msaidizi kwa hivyo anafahamu wachezaji vyema. Tatizo ni hajui jinsi ya kuwatumia,” alidai.

Humphrey Wesonga alisema, “Harambee Stars imeajiri mtu ambaye hafai kabisa kuwa kocha wake.”

Matelong Ngoitoi Malinson, “Hakuna cha kujivunia kuhusu timu hii, Kimanzi, katika hatamu yake, hajashinda mechi hata moja.”

Sammy Ndiema, “Harambee Stars ilikosa ilipomchagua Kimanzi kuwa kocha mkuu.”

Baadhi ya mashabiki wanataka Harambee Stars ivunjiliwe mbali. Alisema Tsuma Saro Edward, “Tuvunje Harambee Stars na tumakinike zaidi katika riadha.”

Boniface Lumbasia alielekeza hasira yake kwa wachezaji. Anasema, “Wachezaji wote walisikitisha na hawastahili kulipwa mshahara na timu ya taifa. Timu hii inafaa kuvunjiliwa mbali. Inakuwaje inatuharibia wikendi yetu?